Pepo la utekaji nyara vijana wanaokosoa serikali!
SERIKALI iliendelea kulaumiwa kuhusiana na misururu ya visa vya utekaji nyara wa vijana wanaharakati na wanablogu huku Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja akikana madai kuwa maafisa wake ndio wahusika.
Viongozi wa kisiasa, wale wa kidini na familia za waliotekwa walishinikiza mateka hao waachiliwe huru au wafunguliwe mashtaka kortini ikiwa wanahusishwa aina yoyote ya uhalifu.
Seneta wa Busia Okiyo Omtatah aliwashutumu maafisa fulani wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI), ambao hakuwataja, kwa kumteka nyara mchora vibonzo Gideon Kibet, almaarufu Kibet Bull.
Kwenye kikao na wanahabari afisini mwake mtaa wa Upper Hill, Nairobi, Bw Omtatah alieleza kuwa Kibet alitekwa nyara baada ya kuondoka afisini mwake Jumanne, Desemba 24, 2024.
Seneta huyo alisema aliona magari aina ya Subaru nje ya afisi yake siku hiyo alipokuwa akikutana na Kibet na watu wengine wanaoendesha mipango yake ya kuwania urais 2027.
“Naamini alitekwa nyara na maafisa wa DCI. Punde tu alipofika afisini mwangu walinzi wangu waliniambia walikuwa wakichunguza gari moja aina ya Subaru iliyowekwa vifaa vya kunasa mawasiliano. Gari hilo lilisalia hapo na likaondoka baada ya Kibet kuondoka,” Seneta huyo anayepania kuwania urais 2027 akaambia wanahabari, akisema ni baada ya hapo ambapo ilibainika kuwa Kibet alitoweka.
Bw Omtatah alishikilia kuwa Bw Kanja na Mkurugenzi Mkuu wa DCI Mohamed Amin ndio wanapaswa kuwajibikia kutekwa nyara kwa Kibet na vijana wengine siku za hivi karibuni.
Awali, Bw Kanja alikana madai kuwa polisi wanahusika katika visa vya utekaji nyara wa wanaharakati hao wa kizazi cha Gen Z.
Wengine ni; Peter Muteti aliyetekwa nyara eneo la Uthiru, Nairobi, Bill Mwangi aliyetekwa mjini Embu, Bernard Kavuli na Steve Mbisi alichukuliwa kwa nguvu eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos, Jumatano siku ya Krismasi.
Hata hivyo, Bw Kanja hajaelezea ni kwa nini maafisa wake hawajawakamata “wahalifu” hao ambao wamekuwa wakiwateka nyara vijana hao kwa kusambaza jumbe na vibonzo vinavyowadhalilisha viongozi wakuu serikalini.
Kwenye taarifa, Inspekta Jenerali wa polisi alisema hamna kituo cha polisi nchini kinachomzuilia mtu yeyote aliyeripotiwa kutekwa nyara.
“Maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) hawahusiki katika vitendo vyovyote vya utekaji nyara, na hamna kituo chochote cha polisi nchini kinachozuilia watu hao walioripotiwa kutekwa,” akasema.
Bw Kanja alieleza kuwa kazi ya polisi ni kuwakamata washukiwa wa uhalifu, kuzuilia katika vituo vya polisi na kisha kuwawasilisha kortini ili wafunguliwe mashtaka.
Aliongeza kuwa Mamlaka ya Kufuatilia Utendakazi wa Polisi (IPOA), na asasi nyingine husika, zinachunguza visa hivyo, huku akitoa wito kwa umma kutoa habari kuhusu mtu yeyote aliyetoweka, kwa kituo cha polisi kilicho karibu.
Hata hivyo, IG alionekana kujikanganya kudai kuwa maafisa wake hawahusiki na visa hivyo anavyokiri kuwa vinachunguzwa na IPOA.
Sababu ni kwamba kulingana na sheria iliyounda IPOA, wajibu wa mamlaka hiyo ni kuchunguza vitendo vya ukiukaji sheria miongoni mwa maafisa wa polisi wala sio raia.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ameitaka serikali kukomesha visa hivyo vya utekaji nyara akivitaja kama “vitendo vilivyopitwa na wakati.”
Akiongea alipohudhuria ibada ya Krismasi, Jumatano, katika Kanisa la Kianglikana (ACK) la Nyamira, Bondo, kaunti ya Siaya, Bw Odinga alisema kuwa visa kama hivyo haviwezi kuruhusiwa kutokea nyakati kama hizi kwani vinarejesha nchi katika enzi za kale ambapo vitendo kama hivyo vilikithiri.
“Tunataka nchi tulivu na yenye usalama. Hizi sio nyakati wa kukamata na kukuzuilia mtu katika vyumba vya Nyayo House. Inasikitisha kuwa siku hizi unapelekwa kusikojulikana. Ni vitendo vilivyopitwa na wakati na havikubaliki,” akasema.
Naye kiongozi wa Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK) Jackson Ole Sapit alitaja utekaji nyara kama “vitendo wa kishetani.”
Kwenye ujumbe wake wa Krismasi aliitaka serikali kuamuru kuachiliwa huru kwa waliotekwa au washtakiwe kwa mujibu wa sheria.
“Visa hivyo vya vijana kutekwa nyara kiholela vikomeshwe. Hivi ni vitendo vya kishetani ambavyo havifai kuendelea kushuhudiwa nchini. Tunataka nuru mpya tukielekea kuingia mwaka mpya na hivyo serikali iachilie waliotekwa,” akaambia wanahabari baada ya kuongoza Ibada ya Krismasi katika Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi.