Bloga matatani kusema wanawake wasiavye mimba ya ubakaji
MASHIRIKA Na PETER MBURU
BLOGA mmoja tatanishi amekashifiwa vikali, baada ya kusema kuwa wanawake hawafai kuavya mimba wanazopata kwa kubakwa, akisema hiyo ni kulipiza ubaya kwa ubaya.
Mama huyo wa watoto wanne Mmarekani ambaye amekuwa bloga anayejiita mke aliyebadilika aliwasihi wanawake kuwaza tena wanapotaka kuavya mimba, kupitia ujumbe wa Facebook.
Alipoulizwa ikiwa mwanamke anafaa kulazimishwa kubeba mtoto wa mbakaji na mmoja wa mashabiki wake, alisema kuwa “Ubaya kwa ubaya hauna faida.”
Ni kweli kuwa wadhulumiwa wa kingono huwa na huzuni, na zaidi wanapoachwa na uja uzito. Lakini baadhi ya mashabiki wa bloga huyo walihoji kuwa anayebakwa bado anawezakuamua kujifungua na kupeana mtoto alelewe na mtu mwingine ikiwa hawataweza.
Lakini baadhi ya wanawake hawakufurahishwa na matamshi ya bloga huyo, wakimkashifu vikali.
Wengine walianzisha mjadala mkali mitandaoni na kupendekeza kuwa hata wanaume wanaowalipia wapenzi wao pesa za kuavya mimba wanafaa kulaumiwa.
Bloga huyo amewahi kughadhabisha watu tena, wakati alidai kuwa wanaume hawawezi kuoa tena kwa kuwa wanawake wamejichafua. Alitaja hali ya wanawake kuavya mimba kuwa ‘kuua’.