Habari Mseto

Wamiliki wa jengo lililoporomoka washtakiwa kwa mauaji

January 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na RICHARD MUNGUTI

WAMILIKI wa jumba la orofa tano lililoporomoka katika kijiji cha Casanova mtaa wa Huruma, Kaunti ya Nairobi wameshtakiwa kwa mauaji.

Bw James Mwangi Maigwa na Teresia Wanjiku Mwangi walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Peter Ooko na kukanusha mashtaka matatu ya mauaji bila ya kukusudia na kujenga nyumba bila idhini ya kaunti ya Nairobi.

Bw Maigwa na mkewe Teresia walikanusha mashtaka hayo manne dhidi yao na kuomba waachiliwe kwa dhamana

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Bw Festus Njue haukupinga ombi la mume na mkewe hao kuachiliwa kwa dhamana.

Wawili hao walikana mnamo Mei 3 2018 katika kijiji cha Casanova mtaa wa Huruma kaunti ndogo ya Starehe walisababisha kifo cha Daniel Karanja Njoroge bila kukusudia.

Shtaka la pili lilisema wawili hao walisababisha vifo vya Eunice Nyakio Karanja na Andrew Musamali.

Shtaka la nne lilisema kuwa wawili hao walijenga jumba hilo la orofa tano bila idhini ya baraza la kaunti ya Nairobi kati ya Januari 2011 na 2015.

“Jumba lililoporomoka inamilikiwa na washtakiwa hawa wawili,” alisema wakili anayewatetea.

Bw Ooko aliombwa awaachilie wawili hao kwa dhamana.

“Washtakiwa wamekuwa nje kwa dhamana ya Polisi. Naomba mahakama iwaachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu kwa vile wawili hawa ni wazazi na ndio wanaotegemewa na watoto wao na watu wengine wa familia zao,” alisema wakili.

Pia aliomba mahakama iwape nakala za mashahidi waanze kuandaa tetezi zao mapema.

Kesi iliorodheshwa kusikizwa Feburuari 25 mwaka huu.

Hakimu aliwaamuru walipe dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni ndipo waachiliwe kutoka rumande.