Wakili aomba kesi ya mauaji ya chifu Marsabit ipelekwe Meru
Na RICHARD MUNGUTI
CHIFU aliyestaafu ni miongoni mwa washukiwa wanne waliofikishwa katika mahakama kuu kwa mauaji ya chifu katika Kaunti ya Marsabit.
Bw Doyo Galgalo (chifu wa zamani), Galma Galgalo , Bi Bokaya Dida Boru na Somo Huka Kanchoro walifikishwa mbele ya Jaji James Wakiaga na kuomba warudishwe katika mahakama ya Meru walipoachiliwa Ijumaa iliyopita.
Na wakati huo huo Jaji James Wakiaga aliamuru Bw Kanchoro apelekwe katika hospitali ya Mathare akapimwe ikiwa akili yake ni timamu kumwezesha kujibu mashtaka ya kumuua Chifu Godana Darara.
Hata kabla ya kesi kuendelea wakili Roger Sagana aliomba mahakama iamuru kesi hiyo ipelekwe katika Mahakama kuu ya Meru ambapo Galgalo, Galma na Dida walikuwa wameshtakiwa mbele ya Jaji Ong’injo.
Washukiwa hao waliachiliwa na Jaji Ong’injo baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma DPP kutatamisha kesi dhidi ya washukiwa.
Punde tu baada ya watatu hao kuachiliwa vurugu ilizuka katika mahakama kuu ya Meru huku watu wa familia ya marehemu wakidai haki itendeke na waliohusika na mauaji ya afisa huyo wa utawala.
“Naomba mshtakiwa wanne Bw Kanchoro kupelekwa kupimwa ikiwa yuko na akili timamu kuweza kujibu shtaka dhidi yake,” wakili Roger Sagana alimsihu Jaji James Wakiaga.
Ombi hilo halikuwa kupinga na kiongozi wa mashtaka Bi Jacinta Nyamosi anayemwakilisha DPP katika kesi hiyo akisaidiwa na Bw Kiget Kiprotich.
Jaji Wakiaga alifahamishwa na wakili Sagana kwamba kesi ya mauaji dhidi ya mmoja haiwezi kuendelea bila ya kuwa ripoti ya mtaalam wa tiba za ubongo.
Jaji huyo alimwamuru afisa anayechunguza kesi hiyo ampeleke Bw Kanchoro hospitali kuu ya Mathare akapimwe akili na awasilishe ripoti ya matokeo ikiwa akili yake ni timamu leo.
Vile vile Jaji Wakiaga alimwamuru DPP awasilishe majibu ya madai kwamba anakandamiza haki za washukiwa hao wanne walioachiliwa kwa kukosekana kwa ushahidi dhidi ya washukiwa waliofikishwa mahakamani.
Bw Sagana aliomba kesi dhidi ya wanne irudishwe katika mahakama ya Meru kwani korti hiyo iko karibu na mahala pa tukio la mauaji.
“Kesi zote za kaunti ya Marsabit husikizwa katika mahakama ya Meru. Kesi hii sio spesheli na zile nyingine ndipo iwasilishwe Nairobi.”
Mahakama ilielezwa kuwa polisi wamekuwa wakiomba muda wachunguze mauaji hayo.
Mahakama ilijulishwa washukiwa hao wamekuwa rumande kwa wiki tatu na “kila wakati DPP husema uchunguzi haujakamilishwa.|”
Mahakama iliamuru kila mmoja wa washukiwa hao azuiliwe.