Habari Mseto

Mama amsamehe mumewe aliyemdhulumu kuokoa ndoa

January 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

NA RICHARD MAOSI

Mahakama ya Nakuru, Jumatatu ilimpa afueni raia wa Marekani aliyekabiliwa na madai ya kumpiga na kumjeruhi mke wake mwenye asili ya Kenya.

Matthew Stumpf Herbert (pichani) anayehudumu kama mhandisi wa kutengeneza barabara nchini Marekani, alisimama mbele ya hakimu mkuu Benard Mararo siku ya kusomewa mashataka dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia.

Mke wake Lilian Mwai alimshataki kwa polisi baada ya kujeruhiwa na Matthew.

“Tarehe 17 Januari katika mtaa wa Koinange Nakuru Magharibi,mshatakiwa alimpiga vibaya mke wake na kumwachia majeraha mabaya,” kiongozi wa mashataki alisema.

Mshatakiwa alikiri makosa lakini akasema mkewe alikuwa tayari kumwondolea madai yaliyokuwa yakimkabili.

Bi Mwai alikubali kumsamehe akaahidi kupatana na mume wake.

“Mshtakiwa amekiri makosa yake na sina budi kumpatia nafasi ya pili. Tumejaliwa mtoto mmoja anayehitaji uangalizi wa wazazi wote wawili,” alisema.

Bw Mathew anasema alijutia makosa yake na alikuwa tayari kurejesha uhusiano na familia yake iliyoanza kumtenga.

Licha ya mahakama kumdadisi Bi Mwai endapo angebadilisha mawazo kabla ya kumwondolea Matthew mashataka, alihakikishia mahakama kuwa alikuwa ameamua kumsamehea.

Kulingana na Bi Mwai mume wake alikuwa ni mtu mzuri kinyume na jinsi watu walivyomchukulia.

“Tunakubali hatua ya mlalamishi kuondoa kesi, mshatakiwa yuko huru kuanzia sasa,”aliamua hakimu Mararo.