Habari

Nafasi yatolewa ya kurudia KCSE iwapo hukuridhika kabla mtihani huo kufutwa kabisa 2027

Na CHARLES WASONGA January 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SASA watahiniwa ambao walikosa kufanya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE), kutokana na sababu mbalimbali, wataweza kuufanya mtihani huo katikati mwa mwaka.

Hii ni baada ya Wizara ya Elimu kutangaza kuwa KCSE hiyo ya katikati mwa mwaka, itafanyika mwezi wa Julai.

Akitangaza matokeo ya KCSE ya 2024, Alhamisi, Januari 9, 2025, Waziri wa Elimu Julius Migos Ogamba alisema hatua hiyo imechukuliwa kuimarisha ubora wa mfumo wa mitihani ya kitaifa.

“Kuanzia mwaka huu, na baada ya kufanya mashauriano na wadau, ningependea kutangaza kuwa Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (KNEC) limeanzisha mtihani wa KCSE ya katikati mwa mwaka utakaofanywa Julai kila mwaka,” akaeleza katika makao makuu ya KNEC, Nairobi.

“Mtihani huo utalenga watahiniwa ambao wangependa kurudia KCSE baada ya kutoridhishwa na matokeo waliyopata na wale waliokosa kufanya mtihani huo baada ya kuugua au kukumbwa na changamoto zisizotarajiwa,” Bw Ogamba akaeleza.

Waziri aliongeza kuwa KCSE hiyo ya katikati mwa mwaka pia inalenga watu wazima ambao wangetaka kupata cheti cha mtihani huo.

Bw Ogamba pia aliongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuwafaidi wanafunzi wenye mahitaji mbalimbali huku ikihakikisha kuwa wote wanapata elimu kwa usawa na urahisi.

Katika miaka ya nyuma, watahiniwa waliokosa kufanya KCSE, baada ya kusajiliwa, kutokana na sababu mbalimbali katika vile ugonjwa, walilazimika kusubiri hadi mwaka unaofuatia kuufanya mtihani huo.

Aidha, wale ambao walitaka kurudia KCSE baada ya kupata gredi isiyowaridhisha pia walilazimika kurudia masomo katika kidato cha nne na kuufanya mtihani huo mwaka mmoja baadaye.

Kawaida, mtihani wa KCSE hufanywa mara moja mwishoni mwa mwaka.