Makala

Jinsi changarawe huvunwa kila uchao Machakos ila serikali ya kaunti inalia haipati pesa

January 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Machakos hupoteza mamilioni ya pesa kila mwaka kutokana na biashara haramu ya changarawe.

Kulingana na Mwakilishi wa Wadi ya Kalama Bw Boniface Mueke ambaye pia, ni mwanachama wa Kamati ya Mazingira, biashara hiyo haramu imechangia ukusanyaji duni wa mapato kutoka kwa wanaochimba.

Bw Mueke aliongeza kuwa utekelezaji hafifu wa ada za usafirishaji na ushirikiano kati ya kampuni za usafirishaji na ufisadi kutoka kwa maafisa wa serikali wa eneo hilo umechangia pakubwa.

Alifichua kuwa zaidi ya kampuni tatu husafirisha changarawe bila kulipa ada zinazohitajika.

“Kila kampuni husafirisha angalau malori 400 ya mchanga kila siku. Iwapo kila lori lingelipa Sh2,000 kwa kila safari, kaunti ingeweza kupata Sh800,000 kila siku au Sh24 milioni kila mwezi,” alieleza.

Alikashifu makarani katika vituo vya ukusanyaji wa mapato ambao hukabidhi serikali, Sh31,000 tu kwa siku badala ya kiwango kinachopaswa kuwa kikubwa zaidi.

Ardhi iliyoharibika kutokana na uchimbaji changarawe, eneo la Mwala. Picha|Fridah Okachi

Mfanyabiashara wa changarawe Bw Mike Wambua alisema ili kuepuka usimamizi wa maafisa wa kaunti na ada za ziada, usafirishaji mwingi wa mchanga hufanyika baada ya saa 12 jioni, hali inayozuia serikali kupata mapato.

“Lori mmoja huchukua chngarawe kwa Sh5,000. Kati ya hizo, Sh3,600 huwalipa wafanyakazi wangu, Sh500 kwa mmiliki wa ardhi, na kusalia na Sh900 tu,” alisema Bw Wambua.

Utekelezaji sahihi wa kanuni, umeruhusu ufisadi kutawala biashara hiyo. Wafanyabiashara hao, wakitumia udhaifu wa miundo ya utawala katika maeneo hayo.

Mwakilishi wa wachache Bw John Munyao, alisema serikali hiyo, inapania kuhalalisha biashara hiyo ili kupunguza mianya inayopoteza mapato.

“Tunahitaji vikundi vilivyoandaliwa ambavyo vitahakikisha kazi za heshima kwa mishahara inayostahili bila kuwanyonya wananchi wa kawaida,” alisema Bw Munyao.

Alisisitiza umuhimu wa kuwa na maeneo maalum ya kuchimbaji changarawe ili kupunguza madhara ya mazingira na kuhakikisha ustawi endelevu.

Kwa sasa Kamati ya Mazingira ya Machakos, kwa sasa inapendekeza mageuzi ya sera haswa kupitia Mswada wa Fedha ambao utaongeza ada za usafirishaji wa mchanga hadi Sh3,000 kwa kila safari. Pia inapanga kufungua barabara zitakazo wawezesha wateja kufikia vituo halali vya mauzo.