Watatu wafariki baada ya kuangukiwa na ndege Malindi
WATU watatu wamefariki kufuatia ajali iliyohusisha kuanguka kwa ndege ndogo katika kijiji cha Kwachocha huko Malindi kaunti ya Kilifi.
Ndege hiyo iliyokuwa kwenye safari ya kawaida ya mafunzo, inasemekana ilipata hitilafu ya kiufundi, na kuilazimu kutua katika barabara kuu ya Malindi-Mombasa, na kuua mwendesha bodaboda, abiria wake na mtu mwingine aliyekuwa amesimama kando ya barabara.
Kulingana na ripoti ya polisi, ndege hiyo aina ya Cesna 172 ilikuwa ikitoka uwanja wa ndege wa Malindi kuelekea uwanja wa ndege wa Wilson, Nairobi ilipopata matatizo ya kiufundi.
Ripoti ilitaja waliofariki katika ajali hiyo kama mwalimu mmoja wa shule ya msingi, wanabodaboda wawili ambapo mmoja alichomeka kiasi cha kutotambuliwa.
Rubani wa ndege na wahudumu wengine akiwemo aliyekuwa akipatiwa mafunzo waliokolewa na kukimbizwa hospitali.
“Rubani wa ndege na wahudumu wengine wawili waliokolewa na maafisa wa polisi na kukimbizwa hospitali ya Twafiq, Malindi,” ilisema ripoti ya polisi.