Chama cha DP chasema kiko tayari kumhifadhi Gachagua na washirika
CHAMA cha Democratic Party of Kenya (DP), kilichoanzishwa na aliyekuwa Rais Mwai Kibaki, kinasema kiko tayari kumpa hifadhi aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na washirika wake kufuatia mpango wao wa kuondoka chama cha Rais William Ruto cha United Democratic Alliance (UDA).
Chama hicho, ambacho kilikuwa miongoni mwa vile vilivyoundwa mara tu baada ya utawala wa Rais Daniel Moi kurejesha demokrasia ya vyama vingi mnamo 1991, kilisema ushirikiano wake na utawala wa Rais Ruto wa Kenya Kwanza hauwezi kudumu tena kutokana na mtindo wake wa utawala.
“Hata hatuamini kuwa Kenya Kwanza ingalipo baada ya rais na chama chake cha UDA kuamua kuunda serikali iliyojumuisha wanachama wa ODM katika Baraza la Mawaziri. Huo ulikuwa mwisho wa Kenya Kwanza,” akasema Bw Jacob Haji, Katibu Mkuu wa DP na msemaji wa chama hicho.
Alisema ingawa DP haijafanya mazungumzo rasmi na Bw Gachagua, kiko wazi kwa wote, akiwemo naibu wa rais wa zamani. “Gachagua ni gwiji katika siasa za Kenya na hivyo basi, aina ya watu ambao tungependa kuwa nao katika uongozi wa chama hiki. Katiba ya Kenya chini ya Kifungu cha 38 inampa kila Mkenya haki ya kufanya maamuzi ya kisiasa,” Bw Haji aliambia Taifa Leo jana.
Bw Gachagua aliahidi kutoa mwelekeo kwa wafuasi wake, hasa kutoka eneo la Mlima Kenya, kufikia mwisho wa mwezi huu anapotarajiwa kutangaza rasmi chama chake kipya cha kisiasa.
“Mwelekeo utakuwa kuhusu kukimbia usaliti ambao umefanywa kwetu. Utakuwa kuhusu kusema hapana kwa siasa za utumwa. Itakuwa kurekebisha makosa ambayo yalitufanya tumwamini na kumpa Dkt Ruto asilimia 87 ya kura zetu katika mpango usio na mpangilio,” Bw Gachagua aliambia Inooro FM hivi majuzi, kituo cha redio kinachotangaza kwa lugha ya wenyeji wa katikati mwa Kenya.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA