Makala

Kampuni zalemea NCPB kwa ununuzi wa mahindi kwa njia ya ujanja

Na BARNABAS BII January 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAMPUNI za kusaga unga zimebadili mbinu na kukumbatia mbinu bunifu za kuziwezesha kuilemea serikali katika ushindani mkali wa ununuzi wa mahindi kutoka kwa wakulima wakati ambapo kuna uhaba wa zao hilo sokoni.

Baadhi ya kampuni hizo zinatoa vimotisha kama vile bei ya juu, uchukuzi wa mahindi bila malipo kutoka shambani na malipo ya haraka, kwa wakulima ambao wamevumilia bei duni kwa mahindi yao kwa miaka miwili iliyopita.

Kampuni hizo zimeweka matangazo katika maeneo ya umma sehemu kunakokuzwa mahindi katika kaunti za Uasin Gishu na Trans Nzoia zikisema zinanunua mazao hayo kwa Sh3, 850 kwa gunia moja la kilo 90.

Hii ni kutokana na matarajio kuwa kutashuhudiwa uhaba wa mahindi licha ya kupatikana kwa mavuno mazuri ya magunia milioni 60 katika msimu uliopita.

Katika misimu iliyopita, kiwango cha mavuno nchini kilikuwa magunia milioni 41 kwa wastani.

“Tunanunua mahindi kwa bei ya Sh3, 650 kwa gunia la kilo 90 na tunalipa papo hapo. Tuuzie mazao yako,” likasema mojawapo ya matangazo hayo yaliyotundikiwa kando ya barabara ya Eldoret kuelekea Kitale.

Wafanyakazi wa kampuni nyingine za usagaji wameungana na wafanyabiashara wenzao kuanzisha kampeni ya nyumba hadi nyumba kuvutia wakulima wawauzie mahindi badala ya kuuza zao hilo kwa Bodi ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao (NCPB).

Asasi hiyo inalenga kununua magunia milioni moja ya mahindi kwa bei ya Sh3,500 kwa gunia la kilo 90, ya thamani ya Sh3.5 bilioni kwa ajili ya hifadhi ya kitaifa ya chakula.

“Ushindani mkali kati ya kampuni za usagaji na NCPB ambao umechangia bei ya mahindi kupanda utawapa wakulima moyo wa kuwekeza katika kilimo cha mahindi ili wapate faida,” akasema Maria Kosgei kutoka eneo la Sergoit, Uasin Gishu.

Taifa linatarajia kupata mavuno mazuri ya mahindi msimu huu kutokana na mpango wa serikali wa kusambaza mbolea ya bei nafuu na kukomaa haraka kwa mazao kutokana na mvua kubwa iliyoshuhudiwa nchini.

Kaunti ya Trans Nzoia inatarajia kuzalisha magunia milioni 5.3 ya mahindi . Kwa kawaida, kaunti hiyo hutumia magunia milioni 2 kila mwaka huku magunia milioni 3.3 yakitarajiwa kutolewa sokoni.

Kaunti ya Uasin Gishu nayo inatarajiwa kuzalisha magunia milioni 4.5 ya mahindi msimu huu huku ikitoa magunia milioni 2.5 sokoni.

Kufikia sasa, bodi NCPB imenunua karibu magunia 16,000 ya mahindi kutoka eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa huku wengi wa wakulima wakihifadhi mahindi wakitarajiwa kuuza baada ya bei kuongezeka.

“Ni idadi ndogo ya wakulima wanaowasilisha mahindi yao kwa vituo vyetu vya kununua mahindi ili wafaidi kutokana na malipo ya papo hapo,” akasema Titus Maiyo, meneja wa Idara ya Mawasiliano katika NCPB.

Serikali ya Kenya Kwanza imeweka mikakati itakayohakikisha kuwa taifa hili haliagizi mahindi kutoka nje mwaka huu wa 2025.