Afueni bei ya mayai ikiendelea kushuka, wafugaji wakilia hasara
BEI ya mayai nchini inaendelea kushuka licha ya gharama ya malisho kuwa juu.
Punguo hilo, wafugaji wanasema limechochewa na mayai yanayoingia Kenya kutoka nchi jirani.
Mapema mwaka uliopita, 2024, kreti (idadi ya mayai 30) wafanyabiashara wa rejareja walikuwa wakiuzia walaji Sh480.
Bei hiyo inaashiria yai lilikuwa likiuzwa Sh16, wengine wakiuza Sh17.
“Mwaka ulipokaribia kuisha, bei ilianza kupungua; yai likawa Sh15, na sasa ni Sh14,” anasema Susan Njoroge mfanyabiashara wa bidhaa hiyo ya kuku Zimmerman Nairobi.
Susan pia huuza kuku wa nyama, na anadokeza kuanzia mwezi huu wa Januari, 2025, bei ya kuku imeshuka.
“Msimu wa Krismasi, kuku mmoja wa kienyeji aliyeimarishwa tulikuwa tukiuza Sh750 na sasa bei imeshuka hadi Sh700,” anaelezea.
Wapo wafanyabiashara wanaouza kuku Sh600, mmoja, kwa wateja – walaji.
Kufuatia kuingia Kenya kwa mayai kutoka taifa jirani, wafugaji wa ndani kwa ndani nchini wanalalamikia hatua hiyo kuathiri soko.
“Yanapoanza kuingizwa nchini, bei huwa mbovu na mkulima ndiye huishia kubeba mzigo wa hasara,” Kelvin Kilonzo, mfugaji akaambia Taifa Dijitali kwenye mahojiano.
Si mara ya kwanza wafugaji wa kuku kulalamikia kuingia Kenya kwa bidhaa za kuku kutoka mataifa jirani na kuwasababishia hasara kimauzo.
Teresiah Gathii, ambaye hufuga maelfu ya kuku wa mayai anasema kutodhibitiwa kwa bidhaa za kuku kuingia nchini kusipotathminiwa kutahatarisha biashara za waliowekeza kwenye ufugaji.
“Ni muhimu serikali ifahamu gharama ya chakula cha mifugo ingali juu, na sisi wafugaji huumia soko likiwa mbaya,” anateta.
Kukwepa hasara, Teresiah amelazimika kukumbatia mbinu za kujiundia malisho.
Bei ya chakula cha mifugo ilianza kupanda 2020, Kenya ilipothibitisha kuwa mwenyeji wa janga la Covid-19.
Ugonjwa huo, miaka miwili baadaye, Shirika la Afya Duniani ndilo WHO lilithibitisha ulimwengu kuwa huru.
Kushuka kwa bei ya mayai na kuku kukiwa afueni kwa walaji, kwa wakulima wanalia kuendelea kuwa mateka wa hasara.
Aidha, wanapendekeza serikali kutathmini bei ya malighafi ya chakula na pia kupunguza kiwango cha mayai yanayoingia nchini.
Kenya huagiza kutoka nje zaidi ya asilimia 80 ya malighafi kuunda chakula cha mifugo.
Ushuru wa juu unaotozwa malighafi pia unachochea bei kuwa ghali.