Maoni

MAONI: Serikali imetelekeza raia wake wanaoishi ng’ambo kwa hivyo iwakome

Na DOUGLAS MUTUA January 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HIVI majuzi nimeudhika kidogo Rais William Ruto alipotuma pole zake kwa Waamerika ambao ama wamefariki au wakaathirika kwa njia moja au nyingine kutokana na moto unaowaka kwa fujo kwenye jimbo la California.

Nilijiuliza iwapo Dkt Ruto amekwisha kuyashughulikia matatizo yote yaliyo nchini Kenya, miongoni mwayo utekaji nyara, ndipo apate nguvu na muda wa kuwaliwaza watu walio umbali huo.

Wakenya wanaoishi ughaibuni – ingawa wanachukuliwa kama watu waliohamia kwingine na hivyo basi wasiohitaji kushughulika na masuala ya nyumbani – hufuatilia kwa karibu kila kinachoendelea nchini Kenya na husononeka si haba mambo yakienda visivyo.

Baada ya kutafakari kidogo, nilijirudi ghafla, nikajiambia kuwa hakika pole za kiongozi wa nchi ziliafiki kwa sababu Wakenya, ambao ni wapambanaji wa kupigiwa mfano, hupatikana kila pembe ya dunia.

Ukisikia kokote kuna misukosuko, kimbia huko uwajulie hali Wakenya wenzako kwa kuwa haikosi wako huko pia wakisaka riziki. Ndiyo hulka yetu hiyo, kuchakarika ilmradi tu tuitie riziki ya Mungu vinywani, hata katika mazingira hatari.

Walikuwa Ukraine wakati Urusi ilishambulia taifa hilo, walikuwa Iraq, Afghanistan, na kwingineko ambako kumewahi kuzuka vita.

Wakenya ni baadhi ya watu walioathiriwa na moto huo unaoendelea kuteketeza nyumba za watu pamoja na misitu, lakini tunamshukuru Mungu kwamba kufikia wakati wa kuandika makala hii, hakuna Mkenya aliyekuwa amefariki kutokana nao.

Hata hivyo, wapo waliookolewa ila nyumba zao zikateketea, wanaohitaji kusaidiwa ili kuanzisha maisha tena. Moyo wetu wa kusaidiana tungali nao, hivyo wanachangiwa.

Amini usiamini, kwa kuwa moyo wetu wa upambanaji haufi, hao wanaosaidiwa wakati huu watainuka tena na kuanza kuchangia makuzi ya uchumi wa Kenya kama walivyokuwa wakifanya kabla ya kukumbwa na masaibu ya sasa.

Kwa namna fulani, wanategemewa na familia zao zilizo nchini Kenya, hivyo hawana budi kujizoazoa na kuendelea kutafuta jinsi ya kutekeleza majukumu mengi tu ambayo walijitwika walipohamia ugenini.

Rais wa zamani wa Amerika, John Fitzgerald Kennedy, katika hotuba yake baada ya kuapishwa, aliwaambia Waamerika wasijiulize ni kitu gani ambacho nchi yao inaweza kuwafanyia, wajiulize ni kitu gani wanachoweza kuifanyia nchi yao.

Ni sahihi kusema Wakenya walio ughaibuni wameitumikia nchi yao kwa kujituma bila kupata faida yoyote, na sasa ni wakati wao kuuliza ni kitu gani ambacho nchi yenyewe inaweza kuwafanyia.

[email protected]