Habari za Kitaifa

Wandayi amponda waziri mwenzake Muturi akimtetea Haji

Na  GEORGE ODIWUOR January 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI  wa Kawi, Opiyo Wandayi ametoa wito kwa wenzake serikalini kupunguza mashambulizi dhidi ya taasisi ambazo zimepewa jukumu la kudumisha usalama wa taifa.

Bw Wandayi alimtetea Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji ambaye anadaiwa kuhusika na visa vya utekaji nyara ambavyo vimeshuhudiwa nchini kwa muda wa miezi kadhaa iliyopita.

Kulingana na waziri huyo, taasisi kama vile NIS na maafisa wake hawafai kushambuliwa na viongozi wa serikali. Alisema maafisa wa serikali walio na masuala ya kibinafsi wanapaswa kujiepusha na kutamka maneno ambayo yananuiwa kudhalilisha vyombo vya usalama na mashirika mengine yenye jukumu la kuwalinda Wakenya.

“Taasisi zinazolinda usalama wetu wa kitaifa zinapaswa kuepushwa na siasa duni,” alisema. Alikuwa akijibu mwenzake wa Utumishi wa Umma Justin Muturi ambaye Jumanne alidai mwanawe, Leslie Muturi, alidaiwa kutekwa nyara na kuachiliwa na maafisa wa NIS mnamo Juni mwaka jana.

Kulingana na Bw Muturi, alipata taarifa kutoka kwa afisa wa NIS kwamba, mwanawe alikuwa anazuiliwa na shirika hilo kisha akaenda kwa Rais Ruto ndipo akaachiliwa.

Kauli yake imezua mjadala huku baadhi ya viongozi wakitishia kumsuta na kushinikiza ajiuzulu au afutwe.Bw Wandayi alisema viongozi wanapaswa kupima maneno wanayozungumza.

Bila kutaja majina, alisema kauli ya Bw Muturi ilishangaza taifa. “Hata kama tuna masuala yetu binafsi, tunapaswa kuwa waangalifu sana ili kulinda uadilifu wa taasisi zetu. Taasisi zilizo muhimu kama NIS zinapaswa kulindwa dhidi ya matamshi ya kisiasa,” Bw Wandayi alisema.

Alikuwa akizungumza katika Kijiji cha Manyala huko Suba Kusini katika Kaunti ya Homa Bay alipozindua uunganishaji wa stima.

IMETAFSIRIRIWA NA BENSON MATHEKA