Uhuru sasa aonekana kupigia debe azma ya urais ya Matiang’i
HUENDA Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta anapanga kumuunga mkono waziri wa zamani wa Usalama Fred Matiang’i katika kinyang’anyiro cha urais 2027.
Duru zimeiambia Taifa Leo kwamba Bw Kenyatta anashiriki katika mipango ya kuhakikisha kuwa Dkt Matiang’i anazima ndoto ya Rais William Ruto ya kuongoza kwa muhula wa pili.
Mwaka jana vijana wa Gen Z waliopinga utawala wa Dkt Ruto walionekana kuchangamkia azma ya Dkt Matiang’i ya kuwania urais walipotuma jumbe za kumsifia waziri huyo wa zamani.
Na Ijumaa wiki jana, Bw Kenyatta aliwaunga mkono vijana hao akishauri kutoogopa kutetea kile ambacho alitaja kama haki yao na utawala bora.
Rais huyo wa zamani alitoa kauli hiyo siku ambayo wandani wake watatu waliapishwa kuwa mawaziri baada ya uteuzi wao kuidhinishwa na bunge.
Wao ni Waziri wa Kilimo Mutahi Kagwe, William Kabogo (ICT na Uchumi wa Kidijitali) na Lee Kinyanjui (Biashara). Watatu hao waliteuliwa kufuatia mkutano kati ya Rais Ruto na Bw Kenyatta nyumbani kwa rais huyo mstaafu kijijini Ichaweri, Kiambu.
Duru zinasema kuwa Bw Kenyatta ameamua kuunga mkono azma ya urais ya Dkt Matiang’i kutokana na uungwaji mkono ambao waziri huyo wa zamani amepata miongoni mwa vijana.
Katika siku za hivi karibuni, Dkt Matiang’i amekuwa akifanya mashauriano na wanasiasa kadhaa nchini, kama sehemu maandalizi ya kampeni zake.
Kibarua chake cha kwanza ni kuhakikisha anapata uungwaji mkono katika jamii yake ya Gusii, kabla ya kusaka uungwaji maeneo mengine.
Mnamo Jumanne wiki jana, Dkt Matiang’i aliandaa mkutano wa mashauriano na viongozi wa Gusii katika mkahawa wa Fairmont, mtaani Karen, Nairobi ajenda kuu ikiwa ni azma yake ya urais.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka alithibitisha kuwa alihudhuria mkutano huo pamoja na wabunge wengine tisa katika kaunti za Kisii na Nyamira.
Aidha, amewahi kukukutana na wapanga mikakati ya kisiasa na wataalamu wa kisiasa kujadili azma yake.
Mbunge mmoja aliyehudhuria mkutano wa Karen, aliambia Taifa Leo kwamba Bw Kenyatta amemhakikishia Dkt Matiang’i atamuunga mkono na akamshauri kusuka uungwaji kutoka Gusii kwanza.
Mbunge huyo alieleza kuwa Rais Kenyatta pia anapanga kumshawishi kiongozi wa ODM Raila Odinga ajiunge na kambi ya Dkt Matiang’I.
Mwaka jana, Rais Ruto aliwashirikisha wandani wanne wa Bw Odinga katika baraza lake za mawaziri na kuunda serikali jumuishi.
“Mipango thabiti inaendeshwa. Uhuru anajaribu kuwalete pamoja viongozi wa upinzani wamuunge mkono Matiang’i. Yeye ndiye anapanga haya yote,” Mbunge huyo, ambaye aliomba tulibane jina lake, akasema.
Duru zinasema kuwa Bw Kenyatta ambaye awali alikuwa amempendelea Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, amekerwa na ukuruba kati ya makamu huyo wa rais wa zamani na naibu rais wa zamani Rigathi Gachagua.