Ruto: 2026 wakulima wa miwa watapata mbolea inayonawirisha mazao
RAIS William Ruto ameahidi wakulima wa miwa kuwa kufikia mwaka ujao, 2026 watakuwa wakisambaziwa fatalaiza yenye virutubisho kuboresha zao hilo.
Kwa sasa, wanatumia mbolea ya kawaida ambayo pia inatumika kukuza mahindi.
Aidha, wanaendelea kunufaika kupitia mpango wa mbolea ya ruzuku – ya bei nafuu.
Kiongozi wa nchi alisema Jumatatu, Januari 20, 2025 kuwa ataweka mikakati kutafiti mbolea inayolenga kuboresha kilimo cha miwa pekee.
“Lazima tuwe na mpango wa utafiti kupata fatalaiza inayoafikia vigezo vya miwa,” Rais Ruto alisema, akizungumza katika eneo la Mumias, Kakamega ambapo alizindua ugavi wa marupurupu kwa wakulima wa miwa.
Wakulima wa miwa kupata bonasi, ni hatua ya kwanza na ya kihistoria kuwahi kufanyika nchini.
Mbolea ya kipekee ya miwa, Rais alisema itasaidia kuongeza kiwango cha mazao.
Akizungumzia wakulima Mumias, Dkt Ruto alisema mipango aliyoweka inalenga kuona Kenya inauza nje ya nchi zao la miwa badala ya kuendelea kuwa mateka wa uagizaji sukari.
“Maeneo kama vile Nandi, Uasin Gishu na Trans Mara, sasa yamejiunga na orodha ya sehemu zinazolima miwa. Hii ni habari njema,” Rais Ruto alisema.
Nyando, Migori, Mumias na Busia, ni miongoni mwa maeneo tajika katika uzalishaji wa miwa nchini.
Akiahidi kupambana na mabroka katika sekta ya miwa, Rais Ruto alielezea imani yake kwamba kufikia 2027 Kenya itakuwa ikiuza bidhaa za miwa kama vile sukari ng’ambo.
Mwaka uliopita, 2024, Kenya iliandikisha nyongeza ya ekari 42, 000 kukuza miwa, Ruto akisema serikali inalenga kuongeza zingine 200, 000.