Jamvi La Siasa

Ruto anavyoipanga jamii ya Mulembe katika ziara ya wiki nzima jicho likiwa 2027

Na CECIL ODONGO, SHABAN MAKOKHA January 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto amezidisha juhudi za kujenga himaya yake katika eneo la Magharibi akilenga kufidia kura za Mlima Kenya ambazo zinaonekana kumponyoka baada ya aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuondolewa serikalini.

Kuanzia Jumapili, Rais yuko ziarani Magharibi, eneo ambalo limekuwa ngome ya kinara wa upinzani Raila Odinga kwa muda mrefu.

Rais na Bw Odinga ambao walikuwa mahasimu wakuu wa kisiasa katika uchaguzi wa 2022, wameridhiana huku Rais akiunga azma ya waziri huyo mkuu wa zamani kutwaa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Leo, Jumanne, Rais anatarajiwa kuandaa mkutano wa Baraza la Mawaziri katika ikulu ndogo ya Kakamega nyakati za asubuhi, kabla ya kufululiza hadi eneobunge la Shinyalu kuzindua mradi wa kuunganisha umeme.

Malipo ya bonasi

Jana, Rais alikuwa Mumias, Kakamega kushuhudia malipo ya bonasi kwa wakulima wa miwa.

Mnamo Jumapili alihudhuria ibada ya kanisa katika eneobunge la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma ambapo cheche kali za kisiasa zilishuhudiwa.

Kesho, Rais atakuwa katika kaunti za Busia, Kakamega na Vihiga kwa hafla mbalimbali. Ataanza kwa kufungua mradi wa maji wa Lower Nzoia, Busia kisha azindue soko mjini Luanda, Kaunti ya Vihiga.

Mbunge wa Khwisero, Christopher Aseka atakuwa mwenyeji wa Rais anayetarajiwa kufika eneobunge hilo kufungua hospitali iliyopewa jina la mwanasiasa huyo.

Alhamisi atakita kambi kwenye kaunti za Busia na Bungoma kuzindua miradi mbalimbali na kusaka uungwaji mkono.

Rais atatua Alupe, Teso Kusini ambapo atazindua uchimbaji wa bwawa la Alupe kisha azindue mradi wa umeme eneobunge la Nambale.

Kazi hiyo hiyo ya uzinduzi wa mradi wa umeme itampeleka Misikhu, Kaunti ya Bungoma baadaye jioni.

Kutamatisha ziara ya Magharibi

Rais atatamatisha ziara yake Magharibi Ijumaa kwa kufungua soko la kisasa la Chepkule, Bungoma na Bumala, Busia.

Mara ya mwisho ambapo Rais alikuwa Magharibi, ni mnamo Januari 3, 2025 ambapo alifika kwa mechi za fainali za Kombe la Gavana Fernandes Barasa uwanja wa Mumias Sports Complex.

Wiki mbili zilizopita, pia Rais Ruto alikuwa Magharibi wakati wa mazishi ya mamake Spika Moses Wetang’ula eneobunge la Kabuchai ambako cheche kali za kisiasa zilishamiri.

Hapo jana, Rais Ruto alituma onyo kwa wanaoshutumu utawala wake kuwa wajiandae kwa makabiliano makali katika uchaguzi mkuu ujao.

“Kwa sasa namakinikia maendeleo na nitakapoamua kuwakabili kisiasa ndipo wataelewa kile ambacho nimekuwa nikiwafanyia Wakenya.

Wale wanaosaka umaarufu waendelee na jitihada zao ila kwa sasa mimi namakinikia kubadilisha nchi. Wakati mwafaka ukifika, nitamalizana nao asubuhi na mapema,” akasema Rais akiwahutubia raia mjini Mumias.

Ziara hiyo inajiri baada ya ANC, yake Musalia Mudavadi kuvunjwa rasmi na kujiunga na UDA wiki jana, mbinu ambayo inakisiwa inalenga kuhakikisha Rais anadhibiti Magharibi kisiasa.

Takwimu za IEBC

Kwa mujibu wa takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC), kaunti za Bungoma, Kakamega, Vihiga na Busia zilikuwa na jumla ya kura milioni 2.2 mnamo 2022.

Rais pia amekuwa akiwinda kura za Luo Nyanza (Siaya, Kisumu, Migori na Homa Bay) ambazo zina kura milioni 2.1 huku kaunti za Nyamira na Kisii zikiwa na kura 637,010 na 323, 283 mtawalia.

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo anasema hatua ya Rais kukita kambi katika maeneo ya Mulembe na Luo Nyanza ni mbinu ya kuhakikisha kuwa anajaza kura zilizomtoroka Mlima Kenya.

“Rais amegutuka na kugundua kuwa akifuatilia Mlima Kenya atakuwa akipoteza wakati wake bure. Hii ndiyo maana anasaka ufuasi katika ngome za Raila kutokana na kuwa mamlakani kwa serikali jumuishi,” akasema Bw Bigambo.

Hesabu za Rais Ruto ‘ni ngumu’

“Uungwaji mkono huo Nyanza na Magharibi utatokana na kuendeleza maeneo hayo na kukidhi mahitaji ya raia wa maeneo hayo na Kenya kwa jumla. Hesabu za Rais ni ngumu kwa sababu lazima agawanye kura Mlima Kenya na pia apate kura za maeneo mengine yote.

“Itabidi ategemee zaidi ya Mudavadi na Wetang’ula kwa sababu wawili hao hawajaonyesha jitihada za kumvutia ufuasi wa kutosha. Hii ndiyo maana amemsaka Raila na ashiriki miradi ya vijana,” akaongeza.