Maoni

Umoja wa kitaifa ni muhimu kuliko miungano ya kikabila

Na JACKTONE NYONJE January 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MARA nyingi wanasiasa wetu wamekuwa wakihubiri umoja wa raia katika majukwaa ainati.

Baadhi yao wakizungumzia umoja wa kitaifa na wengine wakihubiri umoja wa kikabila kwa mihemko na hisia nyingi kali.

Lakini lengo mara nyingi huwa ni la kisiasa na maslahi ya kibinafsi ya kiuchumi na kijamii.

Utaifa na ukabila ni dhana za utambulisho ambazo zina historia ndefu zilizofinyangwa ili kuibua chuki, ujahili pamoja na ubaguzi wa kimbari.

Ni dhana za miundojamii zinazojengwa, kuimarishwa na kuenezwa na kundi dogo la wanajamii linalolenga kuwagawanya watu ili liwatawale na kuwanyonya watu hao bila pingamizi.

Na pale pingamizi huzuka inazimwa kwa urahisi kupitia propaganda zilizo na misingi yake katika bunilizi hizi za utambulisho wa kijamii.

Au huzimwa kwa mabavu kwa sababu kikundi hicho kimepata uungwaji wa wanajamii wengine ambao tayari huwa wamekengeushwa kwa kuzibwia propaganda na kasumba hizo potovu.

Propaganda huwa ni bangi ya halaiki ambayo huvuruga uwezo wa kufikiria au huyeyusha kabisa ubongo na kuwasaza wanajamii na mabafuru ya vichwa yasiyo na tafakuri.

Kwa hivyo izukapo mizozo ya kikabila na kimbari, hawa waliopika majungu ya chuki na kuyarindima magoma ya vita hujitokeza kama wahisani wakipukutikwa na machozi ya mamba wakihubiri umoja wa kitaifa.

Kama kunguru wakiwaokota panzi wa vita na kuwatumbukiza katika vikaango vya mafuta yanayotokota tayari kwa dhifa zao. Ni mbinu iliyotumiwa na wakoloni kuwateka bakunja Waafrika ambayo ilibuniwa na kuenezwa na wanafalsafa wa Kimagharibi ili kuhalalisha ukoloni na biashara ya utumwa.

Badala ya kusheni lawama wakajibadilisha kilumbwi na kuwasukumizia lawama Waafrika na Warabu na wao wakajisawiri kama wahisani na jeshi la Mungu lililojitolea mhanga kuangamiza utumwa!

Kuhubiri umoja wa kikabila imekuwa mbinu ambayo imetumiwa na tabaka la wanasiasa na baadhi ya wasomi kujinyakulia madaraka na vyeo serikalini.

Tabaka hili limefaidika pakubwa kutokana na miundo mbinu ya kijamii iliyosazwa na wakoloni.

Wasomi na wanasiasa waanzilishi baada ya uhuru waliandaliwa kuhudumu na wala siyo kutumia uwezo wao wa kufikiria kukabiliana na changamoto zinazoikumba nchi na kuzalisha mali.

Mbegu za uhasama wa kikabila zilipandwa enzi hizo za ukoloni na kurutubishwa hadi zikakomaa baada ya uhuru. Makabila yalikuwa yamewekewa vitambulisho vya taswira dumifu- ama kabila hili lina huluka ya wizi na utapeli, linguine lina utiifu wa huduma za upishi na ubawabu; lingine lina sifa ya kiburi na ubadhirifu, lingine sifa ya ukatili,uhayawani na ushenzi, na kadhalika.

Hizi ni taswira dumifu ambazo ni hatari sana ambazo mbali na kutishia umoja wa kitaifa zinaweza kuzamisha nchi katika gharika la umwagikaji damu hususan zikikumbatiwa na tabaka hili la wasomi na wanasiasa wanaokamia ulwa, utajiri na madaraka bila ya kufuta jasho.

Aidha, ukiukaji wa sheria na ufisadi utakithiri maana viongozi ‘wanalinda maslahi ya makabila yao’. Kuchukuliwa hatua za kisheria ni kuonewa.