Duru: Waziri Justin Muturi hajakanyaga afisini kwa siku 10 sasa
WAZIRI wa Utumishi wa Umma Justin Muturi – ambaye Jumanne alisusia kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais William Ruto huko Kakamega – hajakuwa katika afisi za wizara yake kwa siku 10 zilizopita, Taifa Leo imebaini.
Bw Muturi pia alikosekana wakati wa kuapishwa kwa Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Umma katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta (KICC) mnamo Januari 20.
Ingawa PSC ni tume huru, iko chini ya wizara yake.
Duru kutoka Ikulu na Wizara zilithibitisha kwamba Bw Muturi hajaingia ofisini kufuatia kikao chake na wanahabari mnamo Januari 12, ambapo alishutumu serikali kutokana na visa vya utekaji nyara.
Pia alihusisha moja kwa moja Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) na kutekwa nyara kwa mwanawe Leslie Muturi alipofika mbele ya Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) siku iliyofuata.
Lakini Muturi aliambia Taifa Leo kwamba amekuwa akitekeleza majukumu yake hata bila kwenda ofisini. Alisema hakuna nyaraka ambazo ziko ofisini mwake zinazohitaji saini yake.
Siku za Jumanne, Baraza la Mawaziri liliidhinisha mpango wa Mafunzo Kazini katika Utumishi wa Umma ambazo zilitoka kwa Utumishi wa Umma. Bw Muturi alisema yeye ndiye aliyetia saini hati hiyo kabla ya kuwasilishwa kwa Baraza la Mawaziri kujadiliwa katika Ikulu ndogo ya Kakamega.
Alitoa mfano wa Rais Ruto, ambaye kwa sasa yuko katika ziara ya kikazi eneo la Magharibi, akiuliza ikiwa Rais pia anafaa kulaumiwa kwa kutokuwa Ikulu.
“Nimekuwa nikifanya kazi zangu. Kazi sio kuwa ofisini. Lakini nikihitajika pia kimwili, utaniona pia huko. Hakuna kazi moja iliyokwama kwa sababu ya kukosa kwangu ofisini,” Bw Muturi aliambia Taifa Leo.
“Waulize hao watu wanaosema sijafika ofisini wakuambie ikiwa kuna stakabadhi yoyote inayosubiri saini yangu. Hata nilipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hungepata stakabadhi yoyote kwenye meza yangu.”
Kuhusu ni kwa nini alisusia kuapishwa kwa makamishna wa PSC, Bw Muturi alisema kuwa haiko katika ‘maelezo yangu ya kazi kuhudhuria kuapishwa na kupigia watu makofi’.
“Je, kutokuwepo kwangu kulizuia kuapishwa kwa makamishna? PSC ni tume huru. Waziri si mwanachama wa tume. Kuapishwa kwao haikuwa kazi yangu, ni kazi ya mahakama na wale waliokuwa wanaapishwa, kuna mtu anataka niende kusimama pale nipige makofi?” alihoji.
Awali, Bw Muturi alikuwa ametuelekeza kwa Katibu wa Baraza la Mawaziri Mercy Wanjau kuhusu kutokuwepo kwake katika kikao cha Baraza la Mawaziri.
Taifa Leo iliwasiliana na Bi Wanjau, ambaye hakujibu maswali yetu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA