Maoni

Sifa maridhawa za waja wema wa Mwenyezi Mungu

Na HAWA ALI January 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu Subhānahu Wata‘āla, swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam, maswahaba wake na watangu wema hadi siku ya Kiyama.

WachaMungu ni wale wanaojitahidi kuishi maisha ya uchaji Mungu na utiifu kwa Mwenyezi Mungu, wakifuata maamrisho yake na kuepuka makatazo yake.

Katika Qur’ani Tukufu na Hadithi za Mtume Swallallahu Alayhi Wasallam, tunajifunza sifa mbalimbali zinazowatofautisha wachaMungu na watu wengine.

Miongoni mwa sifa za wachaMungu ni imani thabiti kwa Mwenyezi Mungu. Wanamwamini Mwenyezi Mungu kwa dhati na wanayakubali mafundisho yote aliyoteremsha kwa Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam.

Hawafuati tu dini kwa maneno, bali wanaitekeleza kwa vitendo na kuwa mfano wa kuigwa. Wanamtegemea Mwenyezi Mungu pekee kwa msaada, na moyo wao umejaa kumkumbuka Allah kila mara.

WachaMungu pia ni watu wa tabia njema na maadili ya hali ya juu. Wanajiepusha na dhambi kama kusema uongo, kufitini, kusengenya, au kudhulumu. Badala yake, wanajitahidi kuhimiza mema na kushiriki katika mambo yanayowanufaisha wengine.

Waislamu wa Masjid Nur Kijiweni wasikiliza darsa kuhusu sira ya Mtume Muhammad. PICHA | HAWA ALI

Mwenyezi Mungu ameelezea wachaMungu katika Qur’ani: “Na wanatoa mali zao wakiwa wanapenda, kwa jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri…” (Surah Al-Baqarah: 177).

Sifa nyingine ni kusimamisha swala kwa unyenyekevu. WachaMungu wanajua kuwa swala ni nguzo ya dini, hivyo wanatekeleza swala tano kwa wakati, wakizingatia sheria na adabu zake.

Swala kwao ni njia ya kuimarisha uhusiano wao na Allah na kujikumbusha lengo lao kuu maishani, ambalo ni kumridhisha Mwenyezi Mungu.

WachaMungu pia ni watu wenye subira na moyo wa kusamehe. Wanavumilia changamoto za maisha, wakiamini kuwa kila jambo lina mpango wa Allah. Wanajiepusha na hasira na wanajitahidi kulipa ubaya kwa wema. Mwenyezi Mungu amesema: “…na wanaosamehe watu…” (Surah Aal-Imran: 134).

Zaidi ya hayo, wachaMungu wanajitahidi kujiepusha na haramu na mashaka. Wanahakikisha kuwa riziki yao ni halali na kwamba matendo yao hayamchukizi Mwenyezi Mungu.

Kwa kumalizia, wachaMungu wamepewa bishara ya neema kubwa katika Akhera. Mwenyezi Mungu amesema: “Bila shaka wachaMungu watakuwa katika Bustani za Pepo na chemchemi.” (Surah Adh-Dhariyat: 15). Tuombe Allah atujaalie sifa hizi ili tuwe miongoni mwa wachaMungu.