Akili Mali

Aliacha kazi ya uhasibu kuuza omena Mombasa na hata hajuti

Na CHARLES ONGADI January 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

ULAJI wa samaki aina ya dagaa ama ‘omena’ umekumbatiwa na wengi katika miaka ya hivi punde, huku wengi hasa mitandaoni wakionyesha njia mbalimbali za kuwaandaa.

Katika soko la Kongowea Kaunti ya Mombasa, kumetengwa eneo maalum ambako wateja kutoka sehemu tofauti Pwani hufika kununua bidhaa hii.

Hapa wafanyibiashara wadogo kutoka sehemu mbali mbali Pwani hufika kununua bidhaa hii kutoka kwa wafanyibiashara wa jumla kwa lengo la kuwauzia wateja wao mitaani kwa bei ya rejareja.

Wilkista Atieno Oricho, 36, ni kati ya wafanyibiashara maarufu wa dagaa wanaopigiwa mfano katika soko la Kongowea.

Kila asubuhi wateja kutoka maeneo tofauti Pwani humiminika katika kibanda chake kununua bidhaa hii inayotumika kama kitoweo na wakazi wengi.

“Nililazimika kuwacha kazi kama mhasibu katika kampuni ya Kenya Pipeline kuzingatia biashara hii ya samaki aina ya Omena baada ya kugundua faida yake,” asema Wilkista katika mahojiano na AkiliMali.

Mara baada ya kukamilisha masomo yake ya kidato cha sita katika Shule ya Upili ya Tororo nchini Uganda mwaka wa 2007, Wilkista alijiunga na Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa alikosomea uhasibu.

Baada ya kuhitimu aliajiriwa kama mhasibu katika kampuni ya Kenya Pipeline kazi aliyodumu kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kujiuzulu na kujitosa katika biashara.

“Kazi ya kuajiriwa ina sheria na masharti ya kuzingatiwa kila mara na hili lilinikosesha utulivu moyoni na nikaamua kupiga moyo konde na kujitosa katika biashara,” asema Wilkista.

Asema mamake mzazi alikuwa muuzaji samaki katika soko la Kongowea kabla ya kuamua kurudi nyumbani eneo bunge la Ugenya.

Safari yake

Anafichulia AkiliMali kwamba alipokuwa angali Shule ya Upili, alifuatilia kwa makini biashara ya mamake na kila mara alifanya utafiti wa namna ya kuweza kuboresha zaidi biashara hiyo.

Wilkista anasema alipata mtaji kutoka kwa akiba aliyojiwekea alipokuwa ameajiriwa na hilo lilimwezesha kuanzisha biashara yake.

Alianza kwa kuagiza gunia moja la dagaa kutoka eneo la Sindo Kaunti ya Homa Bay kwa Sh11,000 na baada ya kipindi kifupi tu alianza kuona matunda ya kazi yake.

“Nilianza kuwauzia wateja wangu kwa bei ya rejareja na baada ya biashara kuanza kunawiri nilibadilisha mtindo na kuamua kuuza rejareja na kwa jumla,” anaeleza.

Baada ya kuona mafanikio Wilkista asema, alianza kuagiza kwa wingi magunia ya dagaa kutoka kwa wavuvi kutoka maeneo ya Sindo, visiwa vya Migingo, Remba na Takawiri Kaunti ya Homa Bay na hata kutoka nchi jirani ya Uganda.

Aidha, Wilkista asema licha ya bei ya gunia kupanda maradufu kulingana na miaka ya nyuma, hilo kamwe halimkoseshi usingizi kutokana na kwamba angali anapata faida.

Anasema kwamba huuziwa gunia moja kwa Sh40,000 hususan kutoka Uganda huku akinunua gunia moja kwa Sh30,000 kutoka kwa wavuvi wa humu nchini.

Ukubwa wa magunia ya dagaa

Mfanyabiashara huyu, anasema tofauti ya bei hutokana na ukubwa wa magunia kutoka Uganda ikilinganishwa na ya humu nchini ambayo huwa ni madogo.

Wilkista anasema kwa sasa ana uwezo wa kuagiza magunia kati ya 10 hadi 15 kwa wakati mmoja kwa kati ya Sh30,000 na 40,000 kwa gunia.

Kutokana na wingi wa wateja, ana uwezo wa kuuza gunia moja kwa siku na kutia kibindoni faida ya kati ya Sh8,000 hadi Sh10,000.

Kuna dagaa ambazo zina mchanga zinapoliwa wakati zingine zikiwa zimeoza ambazo mara myingi wateja hukataa kununua.

“Siri ya kupata wateja wengi ni kufahamu aina ya dagaa inayopendwa na vipimo ninavyotumia bila kutumia njia ya mkato.”

“Ninauza kwa vipimo kuanzia Sh100, Sh150 na Sh1,500 na wale wa jumla wanaonua kwa magunia,” asema kwa bashasha mfanyibiashara huyu.

Mama huyu wa watoto wawili anaiambia AkiliMali kwamba wala hajuti kuwacha kazi ya uhasibu akisema biashara ya dagaa inampatia faida bila ya presha ambayo mara nyingi hutokea katika kazi ya kuajiriwa.

Wilkista anawashauri akina mama kujitokeza kwa wingi kufanya biashara badala ya kutegemea waume wao kuwafanyia kila kitu katika maisha yao ya kila siku.