Shangazi Akujibu

Shangazi, tumejaribu mara kadhaa ila mpenzi ameshindwa kumudu mechi

Na JANE WANGENGE January 31st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Nimeshindwa kusubiri ndoa nikaamua kumpakulia asali mpenzi wangu. Lakini tumejaribu mara kadhaa na ameshindwa. Ninahisi hanipendi.

Hiyo ni hali ya kuvunja moyo hasa unapojitolea kuthibitisha mapenzi yako kwa mwenzako. Lakini ondoa mawazo kuwa hakupendi. Huenda hali hiyo inatokana na wasiwasi. Mpe muda. 

Nashuku mchumba ananicheza na rafiki yangu
Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mwili. Lakini nimegundua yeye na rafiki yangu wa karibu wamekuwa wakinicheza. Najua nikimuuliza atakana. Nifanyeje?

Kama una hakika kuhusu jambo hilo, kuna namna mbili za kupata ushahidi. Kama kweli ni wapenzi, utapata mawasiliano yao kwa simu yake. Chunguza pia mienendo yao uone kama utawafumania.

Demu anapenda pesa kuliko mapenzi ninayompa!
Kuna mwanamke nimekuwa nikimwinda kwa muda mrefu na hatimaye nimemnasa. Lakini nimegundua hatutaenda mbali. Ana mahitaji mengi ya pesa nami sina uwezo.

Shauriana na mpenzi wako umwelezee hali yako kisha ujue iwapo anaweza kupunguza mahitaji yake. Kama hilo haliwezekani, itabidi ujiondoe mapema utafute mwingine.

Nilimfungulia buyu mara ya kwanza, ninahofia ameniambukiza ugonjwa wa zinaa
Wiki iliyopita nilimruhusu mpenzi wangu kuonja asali kwa mara ya kwanza. Nashuku aliniambukiza ugonjwa kwani siku mbili baadaye nilianza kuwashwa. Nina wasiwasi.

Huenda hayo yakawa maambukizi ya aina fulani. Inawezekana kuwa yametoka kwake ama kwako kutokana na kitendo hicho. Ni muhimu umfahamishe pia kisha mtafute matibabu haraka.