Kutopata matibabu kwa wakati chanzo vya vifo vya wazee- ripoti
MABADILIKO ya mtindo wa maisha, gharama ya juu ya huduma za afya na changamoto za kijamii na kiuchumi zimechangia pakubwa katika ongezeko la vifo miongoni mwa wazee nchini.
Hali hii sasa imezua wasiwasi mkubwa kuhusu ubora wa huduma za afya na ustawi wa jumla wa wazee nchini.Data ya hivi punde kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS) inaonyesha kuwa, nimonia, saratani, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo na mishipa ni chanzo cha vifo miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Ripoti ya Kenya Vital Statistics ilionyesha kuwa, kati ya 2019 na 2023, magonjwa haya manne yalisababisha vifo 23,837 miongoni mwa watu wazima, huku nimonia ikiwa hatari zaidi, iliyosababisha vifo vya watu 7,878 mnamo 2021.
Saratani ndiyo chanzo kikuu cha vifo mwaka 2019, kwani jumla ya watu 3,203 walipoteza maisha yao kutokana na ugonjwa huo. “Kikundi hiki cha umri ni hatari zaidi kwa magonjwa yasiyoambukizwa kutoka mtu mmoja hadi mwingine,” inasema ripoti hiyo huku ikisisitiza haja ya haraka ya kuimarisha mifumo ya afya ili kukidhi mahitaji ya afya ya wazee.
Kulingana na ripoti hiyo, magonjwa ya kuambukiza kama nimonia, kifua kikuu na magonjwa ya kupumua pia ni kati ya vyanzo 10 kuu vya vifo nchini.
Dkt James Mwangi alihusisha kuenea kwa magonjwa haya na mabadiliko ya mtindo wa maisha, kucheleweshwa kwa matibabu na miundombinu duni ya afya.
Alisisitiza kuwa nimonia inabakia kuwa wasiwasi mkubwa kwa sababu ya kiwango cha juu cha vifo kati ya wazee, ambao mara nyingi wanakabiliwa na mfumo dhaifu wa kinga na hali ya kiafya, akiongeza kuwa wazee wengi hawapati chanjo ambazo zinaweza kuzuia niumonia, jambo ambalo huwaathiri kiafya.
Kadiri watu wanavyozeeka, kinga zao hudhoofika na hivyo kuwafanya rahisi kupata magonjwa na maambukizi mara kwa mara. Dkt Mwangi alibainisha kuwa wagonjwa wengi wazee hutafuta huduma za matibabu wakiwa wamechelewa, na hivyo kusababisha viwango vya juu vya vifo.
“Mengi ya magonjwa haya yanaweza kudhibitiwa yakigunduliwa mapema, lakini Wakenya wengi hasa wazee hawawezi kumudu uchunguzi wa mara kwa mara au hawayapi kipaumbele hadi matatizo yatakapotokea,” alisema.