Ulaghai wa stima waacha wakazi 100 gizani Kamulu
WAMILIKI wa nyumba zaidi ya 100 katika mtaa wa Green Valley, Kamulu wamesalia gizani kwa juma moja sasa baada ya wafanyakazi wa kampuni ya Kenya Power kukata vikingi vya stima na kutoa nyaya, wakidai kuwa wakazi hao wamekuwa wakitumia umeme usio halali.
Mkazi wa eneo hilo kwa zaidi ya miaka minne, Bi Veronica Wanjiru, alipigwa na butwaa baada ya kufahamishwa na majirani wake kuwa nyaya za umeme zilizounganishwa nyumbani kwake zimekatwa.
Bi Wanjiru alisema kwamba mwaka wa 2016 alitumia Sh203,000 kupata umeme huo, ambao uliunganishwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo kutoka upande wa kushoto wa nyumba yake.
“Nilitembelea jumba la Stima Plaza na kupewa barua iliyoonyesha gharama ya kuunganishiwa. Baada ya kulipa, kampuni hiyo ilituma wafanyakazi wake kuunganisha umeme. Mwaka mmoja baadaye walidai kuwa umeme wangu unapaswa kutoka upande wa kulia, hivyo wakabadilisha,” alisimulia Bi Wanjiru.
Mkazi mwingine, Bi Eunice Wanyaga Njagi, ambaye ameishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 13, alisema kuwa miaka miwili baada ya kuhamia kijiji hicho, alishirikiana na wanavijiji wengine saba kutafuta umeme. Kampuni hiyo iliwaelekeza kutafuta mkandarasi wa kampuni hiyo ili kuwasaidia kupata umeme.
Bi Njagi alisema kuwa kampuni hiyo iliwapatia gharama ya Sh456,000, ambayo ilikuwa ya juu mno.
“Walituhimiza tumtafute mkandarasi. Tulipompata, tulijaza fomu kutoka kwa kampuni hiyo,” alieleza.
Wakati wa operesheni ya kukata nyaya za stima, Bi Njagi alidai kuwa wafanyakazi wa Kenya Power walivamia boma lake na kuchukua mashine ya kusambaza maji, wakidai kuwa ilikuwa inatumia umeme wa wizi.
Katika kijiji cha Athi, eneo la Kamulu, Bi Ruth Wambui ni miongoni mwa waliopata umeme kupitia mpango wa Last Mile Connectivity, uliozinduliwa na serikali kwa lengo la kuhakikisha Wakenya wote wanapata umeme ifikapo mwaka wa 2020.
Bi Wambui alisema kuwa wakati mpango huo ulipoanzishwa, kampuni ya Kenya Power ilifika eneo hilo, kuweka vikingi na kuwaunganisha wakazi na umeme baada ya kulipia Sh30,000.
“Tumekuwa tukinufaika na umeme huo tangu mwaka wa 2017. Wakati wowote stima ikileta hitilafu, kampuni ya Kenya Power imekuwa ikishughulikia,” alisema Bi Wambui.
Wakazi hao walieleza kushangazwa na madai ya kampuni hiyo kuwa umeme wao si halali, ikizingatiwa kuwa vikingi na nyaya ni za kampuni hiyo, na wao hununua tokeni rasmi.
Eneo hilo pia ni hatari kwa wakazi kutokana na uwepo wa wanyama mwitu kama vile chui, ambao huzurura wakati wa usiku. Bw Maina Njoroge alisema kuwa sasa wanalazimika kufika nyumbani mapema kwa hofu ya kuvamiwa na wanyama hao.
Mbunge wa Kasarani, Bw Ronald Karauri, alithibitisha kupokea malalamishi kutoka kwa wakazi wake, akidai kuwa eneo lake limepuuzwa na Kenya Power, huku kampuni hiyo ikihamisha vikingi vya umeme hadi mashambani ili kukamilisha mpango wa Last Mile Connectivity.
“Watu walioletwa na Kenya Power ndio waliweka vikingi hivi. Mimi nimepokea bili kubwa za stima, na kampuni hiyo ni ya kibiashara. Ikiwa gharama ya kuunganishwa ni Sh1 milioni, kwa nini mfanyakazi wao apokee Sh300,000 kwa njia ya mlango wa nyuma ili kuweka stima?” alihoji Bw Karauri.
Taifa Dijitali ilitembelea afisi za Kenya Power tawi la Ruai mnamo Januari 24, 2025. Mmoja wa wasimamizi wake, Bi Faith Wambua, alisema mpango wa kukata umeme huo uliidhinishwa baada ya eneo hilo kukosa mapato yake yanayofaa.
“Kila wakati wakubwa wangu waliona kuwa sisi wafanyakazi hatufanyi kazi ipasavyo. Tulifanya uchunguzi na kubaini kuwa watu wengi wanatumia umeme usio halali,” alisema Bi Wambua.
Aliongeza kuwa wakazi hao waliunganisha umeme kinyume cha sheria, akidai kuwa baadhi ya vifaa vya kununua tokeni katika eneo hilo vilipaswa kutumika katika mtaa wa mabanda wa Mukuru.
“Kwa mfano, mmiliki wa nyumba anaitwa Milcah Njoki, lakini namba ya token inaonyesha kuwa inamilikiwa na James Mburu anayeishi Mukuru,” alieleza msimamizi huyo.