Kindiki ajipata pabaya kulinganisha ufanisi wa Ruto na Kibaki
HUENDA Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki alichokoza nyuki kwa madai yake kwamba Rais William Ruto amepata mafanikio zaidi katika miaka yake miwili ya kwanza kuliko Rais Mwai Kibaki katika miaka yake mitano ya kwanza kuanzia Januari 2003.
Maoni katika mitandao ya kijamii yalikuwa makali, huku wengi wakimshutumu Prof Kindiki kwa kupotosha.
Bw Kibaki, ambaye alimaliza mihula yake miwili mwaka wa 2013 na kufariki miaka tisa baadaye, anasifiwa sana kwa kuiondoa Kenya haraka katika hatari ya kuporomoka kiuchumi, uharibifu wa miundomsingi na taasisi alizorithi kutoka kwa utawala wa Rais Daniel arap Moi wa miaka 24.
Dkt Ruto, kwa upande wake, katika miaka miwili ya kwanza ametatizika kufufua uchumi akisema alirithi deni kubwa kutoka kwa utawala wa mihula miwili wa Rais Uhuru Kenyatta (2013-2022), ambao alihudumu kama naibu wa rais.
Baadhi ya maoni yalipendekeza kuwa hatua pekee ambayo Dkt Ruto alimshinda Kibaki ni utekaji nyara na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu unaofanywa na maafisa wa usalama wa Serikali. Wengi walitoa maoni kwamba Naibu wa Rais, Profesa wa Sheria, amejishusha hadi kiwango cha watu wasio na elimu wanaomsifu Rais.
Muktadha wa simulizi yake ni kuwa utawala wa Ruto katika kipindi cha miaka miwili umeweka msingi wa kiuchumi –ulioleta uthabiti wa Shilingi, mfumuko wa bei kupungua, viwango vya riba na kadhalika – ambavyo alidai kwamba Bw Kibaki hakufanya kufikia mwisho wa muhula wake wa kwanza wa miaka mitano.
Kauli zake haziungwi na takwimu rasmi za Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya, ambazo zinaonyesha kuimarika kwa uchumi kwa haraka punde tu Rais Kibaki alipoyatwaa madaraka.
Prof Kindiki alisema baada ya kurekebisha misingi ya kiuchumi ndani ya miaka miwili ya kwanza, utawala wa Ruto sasa uko mbioni kutimiza, katika miaka miwili ijayo ‘kile ambacho tumezoea kusikia’; “Pato la raia, kuunda nafasi za ajira, mabadiliko ya sekta ya uchumi mdogo ambapo watu wetu wanapata riziki zao.”
Alieleza kuwa Rais Kibaki alirithi uchumi uliokua kwa chini ya asilimia 1 kila mwaka ambao ulipanda hadi asilimia 7 mwishoni mwa muhula wake wa kwanza: “Lakini watu hawali ukuaji. Walikuwa wanamuuliza Kibaki ‘unatuambia kuhusu ukuaji, kuhusu Pato la Taifa, lakini hatuoni kitu’. Maswali yale yale ambayo watu wanauliza leo”.
Aliendelea kulinganisha matatizo ambayo Rais Kibaki alikumbana nayo mwanzoni mwa utawala wake kama vile hali mbaya ya afya, changamoto za upinzani, na muungano uliogawanyika na yale ambayo Dkt Ruto amekumbana nayo.
“Mwaka wa kwanza alikuwa na upinzani mkali kutoka nje,” alisema akizungumzia changamoto alizozipata kutoka kwa kinara wa upinzani Raila Odinga. “Mwaka wa pili Ruto alipata upinzani wa kutisha kutoka ndani ya serikali yake,” alisema akimaanisha matukio yaliyopelekea kuondolewa kwa mtangulizi wake Rigathi Gachagua.
Zaidi ya uchumi, kuna mambo yanayoweza kulinganishwa katika utawala changa wa Dkt Ruto na miaka ya mwanzo ya urais wa Kibaki.Wote wawili waliingia mamlakani kwa miungano ambayo kimsingi ilikuwa mikusanyiko ya makabila – Muungano wa Narc wa Bw Kibaki na muungano wa Dkt Ruto wa Kenya Kwanza.
Prof Kindiki aliwakumbusha wasikilizaji wake historia hii wakati wa mkutano wa Jumatano iliyopita,.Prof Kindiki aliendelea kukumbuka kuwa Dkt Ruto anakabiliwa na changamoto sawa na za Kibaki.
“Kinachoendelea hapa ni kitu ambacho kimetokea hapo awali. Kiongozi yeyote anayeleta mabadiliko lazima afanye maamuzi yasiyopendeza. Viongozi wanaotaka sifa hufanya maamuzi ya kuwaletea maarufu,” alisema.
Huku Bw Kibaki akitekeleza miradi aliyoahidi kama vile elimu ya bure ya shule ya msingi pamoja na upanuzi wa haraka wa mtandao wa barabara –Dkt Ruto ametatizika kutekeleza mpango wa Huduma za Afya kwa Wote (UHC) na mradi wa nyumba nafuu.
Uchumi ulikua kwa kasi wakati Rais Kibaki alipoingia madarakani Desemba 2002 ukilinganisha na kuanzia 2022, Rais Ruto alipoingia Ikulu takriban miaka 20 baadaye.Pato la Taifa lilifikia wastani wa Dola13 bilioni wakati Bw Kibaki alipoingia madarakani, ambayo ni sawa na Dola 113 bilioni ambazo Dkt Ruto alipata miongo miwili baadaye.
Pamoja na kukua kwa uchumi kwa jumla, takriban viashiria vingine vyote, vinaonyesha ustawi thabiti katika miaka miwili ya kwanza ya Bw Kibaki, huku hali ikidoroa kipindi sawia cha Ruto.Kwa upande wa kisiasa, Dkt Ruto anaonyesha imani kwamba atashinda upinzani wote, ambao sasa unaongozwa na Bw Gachagua na masalio ya muungano wa Azimio.
Hata hivyo, hali inabakia kuwa tete. Ukuraba wake na Bw Odinga na kugeukia Magharibi mwa Kenya kupitia Bw Musalia Mudavadi na kujipenyeza Pwani na Kaskazini Mashariki huenda kukakosa kufidia ipasavyo kura nyingi alizopoteza Mlima Kenya.
Kutakuwa na mvutano ndani ya muungano wa Ruto, mirengo ya Raila na Mudavadi itakapoanza kuuliza Prof Kindiki analeta thamani gani ikiwa hawezi kurejesha Mlima Kenya.