Jamvi La Siasa

IEBC mpya itaratibu mipaka kabla ya 2027?

Na CHARLES WASONGA February 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MUUNGANO wa mashirika ya kijamii umesisitiza kuwa uainishaji wa mipaka unaweza kufanywa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilifaa kuratibu upya mipaka ya ndani ya nchi kufikia Machi 2024 lakini hakukuwezekana kwa sababu ya kukosa tume kamili baada ya muhula wa baadhi ya makamishna kupita, wengine kujiuzulu ama kutimuliwa.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi mwishoni mwa wiki, viongozi wa muungano huo kwa jina “Uchaguzi Platform” walipuuzilia mbali hofu ya Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula kwamba zoezi hilo haliwezi kukamilishwa kutokana na kukosekana kwa muda wa kutosha.

Akiongea mjini Naivasha, Bw Wetang’ula alielezea hofu kuhusu uwezekano wa kuundwa kwa maeneo bunge mapya kabla ya uchaguzi ujao, kutokana na kucheleweshwa kwa uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC.

Alieleza kwa kuwa muda wa makataa wa kukamilishwa kwa zoezi ulipita, itakuwa vigumu kwa makamishina wapya kukamilisha shughuli hiyo haraka ili maeneobunge mapya yatumike katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Kutokana na kucheleweshwa kwa shughuli ya uteuzi wa makamishna wapya, haitawezekana kuundwa kwa maeneobunge mapya kuongezea idadi ya sasa ya 290,” Bw Wetang’ula akasema Jumatano alipohutubu katika mkutano wa kukadiria utendakazi wa wabunge kufikia katikati mwa muhula.

Lakini Mshirikishi wa Kitaifa wa Waangalizi wa Uchaguzi (ELOG) Mulle Musau na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuchanganua Sheria za Uchaguzi na Utawala Afrika (ELGIA) Felix Odhiambo wanashikilia kuwa IEBC bado inaweza kuunda maeneobunge mapya.

Mshirikishi wa Kitaifa wa ELOG Mulle Musau akizungumza na wanahabari Jumatano Februari 29, 2025. Picha|Charles Wasonga

“Hili ni suala la kikatiba na Spika Wetang’ula hana mamlaka ya kutoa ufasiri wake kulihusu. Makamishina wapya watakaoteuliwa na jopo ambalo sasa limeanza kazi wanaweza kutekeleza zoezi la uainishaji wa mipaka wakipata ushauri kutoka kwa Mahakama ya Juu. Spika akome kabisa kupoteza matumaini ya Wakenya ambao wangetaka maeneobunge yao yagawanywe ili wapate uwakilishi mzuri,” Bw Mulle akasema.

Kwa upande wake, Bw Odhiambo alielezea imani kuwa makamishina wapya wanaweza kukamilisha zoezi hili akifichua kuwa tayari sekritariati ya IEBC imekamilisha asilimia 60 ya shughuli hiyo.

“Ni asilimia 40 pekee ya kazi ya uainishaji mipaka ya maeneo wakilishi imesalia na makamishina wapya wanaweza kuikamilisha ndani ya muda wa miezi sita baada ya wao kuingia afisini. Kwa hivyo, kiongozi wa hadhi ya Spika Wetang’ula asiibue hofu kwamba huenda baadhi ya Wakenya wakakosa haki yao ya uwakilishi sawa katika uchaguzi mkuu wa 2027,” akaeleza kwenye kikao jijini Nairobi.

Wawili hao, waliandamana na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kupambana na Ufisadi Transparency International, tawi la Kenya, Sheila Masinde na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kutetea Demokrasia ya Vyama Vingi (CMD) Frankline Mukwanja.

Mkurugenzi Mtendaji wa Transparency International Kenya Sheila Masinde akizungumza na wanahabari kuhusu uundaji wa IEBC kabla ya uchaguzi wa 2027. Picha|Charles Wasonga

Kulingana na kipengele cha 89 cha Katiba, shughuli ya uainishaji upya wa mipaka ya maeneo wakilishi inapaswa kufanywa baada ya muda usiopungua miaka minane au kuzidi miaka 12.

Shughuli hiyo ilifanyika mwisho mnamo Machi 2012 ambapo idadi ya maeneo bunge iliongezwa kutoka 210 hadi 290. Idadi ya wadi pia iliongezwa hadi 1, 450.

Kwa hivyo, muda wa mwisho wa kukamilishwa kwa awamu nyingine ya shughuli hiyo ulikuwa Machi 2024.

Lakini, wakati huo IEBC haikuwa na makamishina baada ya kukamilika kwa muhula wa aliyekuwa mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishna Boya Molu na Abdi Guliye mnamo Januari 17, 2023.

Viongozi wa vuguvugu la Uchaguzi Platform pia wameitaka serikali kuu na wabunge kuliunga mkono jopo jipya la uteuzi wa makamishna wa IEBC ili liweze kukamilisha kibarua hicho kwa wakati.

“Tunaamini kuwa kupitia ufadhili mzuri kutoka kwa serikali, kutoingiliwa na viongozi wa serikali na wanasiasa, jopo hilo linaweza kukamilisha kazi yake hata ndani ya miezi miwili,” akasema Bi Masinde.

“Kile ambacho jopo hili linahitaji sasa ni mazingira mazuri na nia nzuri kutoka kwa viongozi wa taifa hili,” Bw Mukwanja akaongeza.

Aidha, walitoa wito kwa serikali kurahisisha taratibu za kupatikana kwa vitambulisho vya kitaifa ili vijana waliofikisha miaka 18 wapate hati hizo kwa urahisi ili wajiandikishe kuwa wapiga kura.

Mkurugenzi Mtendaji wa Centre for Multipuarty Democracy Kenya Frankline Mukwanja katika kikao na wanahabari Jumatano Februari 29, 2025 jijini Nairobi. Picha|Labaan Shabaan