Jamvi La Siasa

Moyo waanza kumdunda Raila, AUC ikibaki siku 10

Na CECIL ODONGO February 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KINARA wa upinzani Raila Odinga anaanza kuhesabu siku 10 leo kabla ya kukabiliwa na mtihani mwingine maishani ambayo itaamua mustakabali na mkondo wa siasa zake.

Bw Odinga atakuwa akiwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) mnamo Februari 15, uchaguzi ambao ushindi utahakikisha siasa zake sasa zinakwezwa hadhi kutoka Kenya hadi Afrika.

Kasi ya mpigo wa moyo wa Raila inatarajiwa kuongezeka ikizingatiwa kufeli kwenye kura hiyo kutamvunia kejeli tele kisiasa baada ya kuanguka urais mara tano mnamo 1997, 2007, 2013 na 2022.

Bw Odinga ambaye amekuwa akiendesha kampeni kali Afrika, amezuru mataifa mbalimbali ambako amekuwa akisaka uungwaji mkono.

Hata hivyo, kasi ya kampeni zake zinaonekana kupungua siku chache zilizopita baada ya mzozo kati ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda kuchipuka.

Hapo awali, Raila alikuwa amejihakikishia uungwaji mkono kutoka ukanda wote wa Afrika Mashariki lakini sasa hilo litategemea jinsi Rais William Ruto ambaye ni mwenyekiti wa EAC atakuwa akishughulikia mzozo huo.

Raila ana upinzani mkali kutoka kwa Waziri wa Masuala ya Nje wa Djibouti Ali Youssouf na mwenzake wa Kisiwa cha Madagascar Richard Randriamandrato.

Hata hivyo, ushindani mkali unaonekana kati ya Bw Odinga na Youssouf.

Kwa mujibu wa sheria ya AU, kuwahi ushindi wa wadhifa huo wa hadhi, mwaniaji lazima apate theluthi mbili za kura kutoka nchi 55 za Afrika ambazo kihesabu ni mataifa 33.

Mara ya mwisho Raila alionekana akimakinikia kampeni za AUC ni Januari 28 ambapo aliungana na Marais wa Afrika katika Kongamano la kuhakikisha kuwa raia milioni 300 kutoka Afrika wanapata umeme kupitia 2020.

Kwenye kongamano hilo, Bw Odinga alionekana akitangamana na kupiga picha na marais mbalimbali, Rais William Ruto akiungana naye kwenye baadhi ya gumzo lililokuwa likiendelea.

Bw Odinga amezuri Kaskazini, Magharibi na Kusini mwa Afrika akisaka uungwaji mkono baada ya Marais wa Afrika Mashariki kuidhinisha uwanizi wake mwaka jana.

Kiongozi huyo wa ODM amepata uungwaji mkono wa zaidi ya nchi 22 na iwapo mshindi hatapatikana kwenye raundi ya kwanza, basi italazimu kura hiyo iamuliwe kwenye raundi ya tatu.

Bw Youssouf naye hajaonekana kwenye kampeni sana duru zikiarifu kuwa amepata uungwaji mkono wa mataifa ya Kiislamu na yale yaliyokuwa chini ya ukoloni wa Ufaransa.

“Hayo matukio ya DRC yasipochukuliwa kwa makini, mengi ya mataifa yatapoteza imani na Kenya.

Rais alikosea kwa kujitokeza na kuzungumzia suala la DRC hadharani ndiyo maana Rais Felix Tshisekedi alikosa mkutano aliouitisha na kuhudhuria lile la SADCC,” akasema Mchanganuzi wa Masuala ya Kisiasa na Mhadhiri Profesa Munene Macharia.

Msomi huyo anaongeza kuwa kuegemea kwa Rais Tshisekedi kwenye mataifa ya Kusini mwa Afrika na uhasama kati ya Rais Cyril Ramaphosa na Rais wa Rwanda Paul Kagame huenda kutavuruga uungwaji mkono kwa Raila AUC.