Ramaphosa anywea, anyenyekea kwa Trump
JOHANNESBURG, AFRIKA KUSINI
RAIS wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa Jumanne aliongea na bilionea wa Amerika Elon Musk kuhusu habari alizodai zilikuwa za uongo na zilizofasiriwa vibaya kuhusu nchi hiyo.
Mazungumzo hayo kwa njia ya simu yalifanyika baada ya Rais Donald Trump kusema atasitisha msaada kwa Afrika Kusini kutokana na sera zake za kibaguzi kuhusu ardhi.
Rais Trump mnamo Jumapili alishutumu Afrika Kusini kwa kutwaa ardhi na kuwanyanyasa watu wa ‘tabaka’ fulani.
Ramaphosa alimjibu kwa kusema serikali haikuwa imetwaa ardhi zozote na sera hiyo ililenga kuwa na usawa katika matumizi ardhi ya umma.
Musk ambaye alizaliwa Afrika Kusini na ni raia wa Amerika, tena mshirika wa Rais Trump, aliingilia mzozo huo, akilaumu Afrika Kusini kuwa na ubaguzi wa rangi hasa inaposhughulikia umiliki wa ardhi.
Alisema wale ambao wamekuwa wakionewa ni watu weupe.
Afisi ya Rais wa Afrika Kusini ilisema Ramaphosa na Musk waliongea kuhusu masuala yaliyoibuliwa ambayo alisema yalikuwa uongo.
Kuongea na Musk imefasiriwa kuwa Ramaphosa amenyenyekea baada ya kumkabili Rais Trump vikali mnamo Jumapili, akisema nchi hiyo haitegemei Amerika.