Habari

Msiwe na hofu kuhusu ubora wa mafuta nchini, zasema KEBS na EPRA

Na GEOFFREY ANENE February 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SHIRIKA la Kukadiria Ubora wa Bidhaa nchini Kenya (KEBS) na Halmashauri ya Kudhibiti Kawi na Mafuta (EPRA) zimepuuzilia mbali uvumi kuhusu usalama wa mafuta nchini, na kusisitiza kuwa petroli ya Super inayouzwa nchini inafikia viwango hitajika vya kitaifa.

Katika taarifa ya pamoja iliyotolewa Alhamisi, Februari 6, 2025 mashirika hayo yalitangaza kuwa sampuli za mafuta zilizochunguzwa kutoka vituo mbalimbali vinavyouza petroli ya 95 Octane Unleaded, zilipatikana kuwa na vipimo vya okteni (RON) vya 96.1, 95.9, 96.0, na 95.9 ambavyo vinaenda sambamba na vipimo vinavyotakikana.

Mashirika hayo ya KEBS na EPRA pia yameonya umma dhidi ya kutumia vifaa visivyo halali au visivyo na vipimo sawa kuchunguza mafuta.

“Tungependa kusisitiza kuwa ni muhimu kutumia maabara yaliyoidhinishwa ili kupata matokeo sahihi ya uchunguzi,” taarifa kutoka mashirika hayo ilisema Alhamisi baada ya ripoti kuibuka kwenye mitandao ya kijamii kwamba mafuta ya Super si salama.