Maoni

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Huu hapa utaratibu bora wa kujiandaa kwa Ramadhani

Na HAWA ALI February 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Yeye ndiye Muweza wa kila jambo, Mwingi wa rehema na mwenye huruma.

Swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad Swallallahu Alayhi Wasallam, maswahaba wake na watangu wema hadi siku ya Kiyama.

Tunaposalia chini ya mwezi mmoja kabla ya kuwasili kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ni wajibu wetu kujitayarisha kimwili, kiroho, na kiakili ili tuweze kufaidi baraka na rehema zake.

Ramadhani si mwezi wa njaa na kiu pekee, bali ni fursa adhimu ya kujikaribisha kwa Mwenyezi Mungu kwa ibada, toba, na matendo mema.

Kwanza, ni muhimu kuanza kujizoesha kufunga hata kabla ya Ramadhani kwa kufunga sunnah kama vile Jumatatu na Alhamisi au ayyamul bi’idh (tarehe 13, 14, na 15 za kila mwezi wa Kiislamu).

Kufanya hivyo kunasaidia mwili kuzoea ibada ya saumu na kupunguza ugumu wa siku za mwanzo za Ramadhani.

Pili, ni muhimu kujitakasa kiroho kwa kutubia kwa dhati.

Tunapaswa kutafakari maisha yetu, kuomba msamaha kwa dhambi zilizopita, na kujitahidi kuacha maovu yote.

Toba ya kweli inapaswa kuambatana na nia ya dhati ya kubadilika na kuwa mtu bora.

Tatu, tunapaswa kuongeza ibada kama kusoma Qur’ani, kufanya dhikri, na kuswali sala za sunnah.

Ramadhani ni mwezi wa Qur’ani, hivyo ni vyema kuanza kuisoma na kuizingatia mapema ili tuwe tayari kuitamatisha au kuisoma kwa wingi wakati wa Ramadhani.

Nne, ni muhimu kujiandaa kimwili kwa kula vyakula vyenye afya na kupunguza vyakula vizito ambavyo vinaweza kuathiri ibada yetu.

Mazoezi ya kiafya pia yanaweza kusaidia mwili kuwa na nguvu ya kuhimili saumu.

Mwisho, tujiepushe na mambo yanayopoteza muda kama michezo isiyo na faida, mazungumzo yasiyo na maana, na dhambi zinazoondoa baraka za Ramadhani.

Tumuombe Mwenyezi Mungu atupe uzima na afya njema tufikie Ramadhani tukiwa tayari, na atujaalie tuwe miongoni mwa wale watakaosamehewa na kufaulu katika mwezi huu mtukufu.