HabariPambo

USHAURI NASAHA: Kuweni na siri, sio kila tatizo la ndoa huambiwa watu wa nje

Na BENSON MATHEKA February 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

NI lazima muweke mipaka ili kulinda ndoa yenu. Watu wengi wanasononeka katika ndoa zao kwa sababu hawajui kuweka mipaka hasa kuhusu habari wanazoshiriki na watu wengine.

Wataalamu wa masuala ya ndoa wanasema ni makosa kuanika kila kitu kuhusu ndoa kwa kila mtu.

“Usishiriki kila kitu kuhusu ndoa yako na watu wa nje. Mambo mengine ya ndoa kama vile raha unayopewa na mtu wako na masuala ya pesa ni matakatifu na ya kibinafsi,” asema David Munyasa, mwanasaikolojia na mshauri wa wanandoa.

Nyumba yenu si soko

Pili, anasema baadhi ya watu wanaruhusu wageni kuingia kila sehemu ya nyumba bila kujua hatari ya kufanya hivyo kwa ndoa yao.

“Watu hawapaswi tu kuingia na kutoka nyumbani mwenu. Nyote mnapaswa kuamua ni nani anayeingia, lini na kwa muda gani. Ni makosa kukubali nyumba yako iwe kama soko ambalo watu wa kila sampuli wanaingia na kutoka wapendavyo,” asema.

Demu akimueleza siri jamaa wake. PICHA | MAKTABA

Zimeni gumzo za kuwadunisha

Tatu, mwanasaikolojia huyu anaonya kwamba watu wakiingilia ndoa yenu huwaacha na kauli zinazowadunisha au kutoheshimu uhusiano wenu.

“Kamwe usivumilie mazungumzo ambayo hayaheshimu ndoa yako au mwenzio. Yaepuke kabisa iwapo unataka kuwa na amani katika ndoa yako,” asema.

Ndoa nyingi, asema, huvurugika watu wakiruhusu maoni kutoka nje ilhali kila ndoa ina changamoto za kipekee. Hivyo basi, anashauri watu kutoamini hata wandani wao wa karibu kuhusu masuala ya ndoa yao.

“Unaweza kuwa mtu wa kupenda kushirikiana na jamii na marafiki, lakini uwe makini usiwaruhusu wawe karibu nawe sana kwani wataathiri ndoa yako. Huu ndio ukweli ambao watu wanapuuza wanapoanika masuala ya ndoa kwa watu wanaodhani ni marafiki au washirika wao katika jamii,” aeleza.

Wachuje makapera na waseja

Mwanasaikolojia Susan Kariuki anasema wanandoa wanafaa kuwachuja marafiki wao wa zamani hasa wale ambao bado ni makapera na waseja.

“Unafaa kuweka mipaka na uwe makini unapofanya hivyo. Jiulize ni thamani gani kila mmoja wa watu hao anaongeza katika ndoa yako,” asema.

Kariuki pia anaonya kwamba ni muhimu mtu kuwa mwangalifu ili kazi yake isiwe na athari hasi kwa ndoa yake.

“Fanya kazi kwa bidii na busara ili kutunza familia yako lakini chunga isikunyime wakati mzuri wa kuwa na familia yako. Sawazisha kazi na familia,” asema Kariuki.

Msianike kila kitu chenu mitandaoni

Muhimu kabisa kwa watu walio katika ndoa, aeleza, ni kuepuka kuamini kila habari na maoni kuhusu ndoa wanazopata katika mitandao ya kijamii.
“Kuna mengi yanayoenezwa duniani na sio yote yenye manufaa kwa ndoa japo yanaweza kuvutia hisia na kuungwa na wengi. Chagua kwa busara. Epuka maoni ya mtandaoni, yamekuwa yakipotosha wanandoa wengi,” asema Kariuki.
Kulingana naye, mapato ya mtu akiingia katika ndoa yanapaswa kuelekezwa kuboresha familia yake kabla ya wengine.
“Ni vizuri kusaidia watu wengine, lakini mnafaa kufanya hivyo pamoja kama wanandoa na kwa hekima mkipatia kipaumbele mahitaji yenu,” asema.