Timu za Kenya zanywea hoki ya Klabu Bingwa Afrika
TIMU za Kenya za wanaume na wanawake zilishindwa kufana katika kindumbwendumbwe cha mpira wa hoki Klabu Bingwa Afrika (ACCC) kilichokamilika jijini Ismailia, Misri.
Vidume vya Nairobi Simba na vijike vya Mombasa Sports Club (MSC) kila moja ziliridhika na nafasi ya nne kwenye mashindano hayo yaliyokunja jamvi Februari 7, 2025.
Nairobi Simba ilimaliza ya pili katika Kundi B ikishindwa kustahimili makali ya Port Fouad ya Misri iliyoilemea magoli 4-3 katika mechi ya kuwania nambari tatu, iliyokuwa kati ya michuano ya mwisho iliyosakatwa Ijumaa. Port Fouad ilimaliza katika nafasi ya pili Kundi A.
Kwa upande wa akina dada, MSC ya kocha Teddy Odada iliridhika na nambari nne baada ya kupoteza 1-0 mikononi mwa Kada Queens ya Nigeria, Ijumaa.
“Imeshakuwa hivyo, tumekubali yaishe. Lakini tumefahamu kwamba tuna uwezo wa kutetemesha Afrika endapo tutapata ufadhili mzuri na kuendelea kujinoa kila wakati,” akasema meneja wa MSC, Angela Okech.
Shindano hilo lilishirikisha timu 20 – kumi za wanaume sawia na za wanawake, zilizopangwa kwa makundi mawili. Mabingwa wa kila kundi walifuzu kwa fainali huku namba mbili ikijinasia tikiti ya kuwania nafasi ya tatu ya jumla kwenye kombe hilo.
Kwenye mechi za Kundi B, Nairobi Simba ilimaliza ya pili na alama saba, mbili mbele ya Ghana Revenue Authority (GRA) ya Ghana. Simba ilisajili ushindi wa mabao 4-3 na 2-0 dhidi ya Zamalek ya Misri na USIU ya Kenya, mtawalia. Kisha iliagana mabao 4-4 na GRA ya Ghana kabla kupepetwa 7-3 na Aircraft Factory ya Misri.
Vipusa wa MSC walianza kwa sare ya 1-1 na Plateau Queens ya Nigeria, wakafinya Wakenya wenzao USIU 1-0, wakagaragaza El Nasr ya Misri 9-0 kabla kufunga kazi 1-0 dhidi ya Smouha ya Misri.
Shindano la mwaka huu lilikuwa la makala ya 35 wanaume na 26 wanawake. Lilishirikisha timu kutoka mataifa ya Kenya, Nigeria, Ghana, Uganda na wenyeji Misri.