Habari

Jinsi mama na mwanawe aliye jela Kamiti walitapeli mtaalamu wa fedha Sh7.6m

Na RICHARD MUNGUTI February 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MTAALAM katika masuala ya kifedha alishtua mahakama ya Milimani aliposimulia jinsi mbakaji anayetumikia kifungo akishirikiana na mama yake walimlaghai zaidi ya Sh7.6 milioni wakidai watamnunulia nyumba ya kibiashara miaka mitano iliyopita.

Akitoa ushahidi dhidi ya Hesbon Onyango Nyamweya na Pamela Akinyi Wara anayezuiliwa katika gereza la wanawake la Lang’ata, Bi Purity Karambu alieleza jinsi alitapeliwa mamilioni hayo ya pesa bila kugundua.

Hesbon alikuwa anapokea pesa akiwa gerezani kisha kumtumia mama yake (Pamela Akinyi Wara) kuziweka kwa benki kwa lengo la kununua nyumba akikamilisha kifungo.

Purity alisema alipoteza kitita cha Sh7,656,500 katika kipindi cha miezi mitano kati ya Mei na Septemba 2020 wakati wa janga la Covid-19.

Purity Karambu akiwa katika Mahakama ya Milimani ambapo alitoa ushahidi katika kesi ya ulagha wa Sh7.6 milionii inayomkumba mama Pamela Akinyi na mwanawe Hesbon Onyango. Picha|Richard Munguti

Purity aliyetoa ushahidi mbele ya hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Bi Susan Shitubi alisema aliangukia kwenye mikono ya walaghai wanaojifanya wafanyabiashara wa kuuza majumba ya kibiashara pamoja na ya makazi.

“Nilitaka kuwekeza katika biashara ya nyumba kukodisha wapangaji au kuweka biashara kama vile duka,” Purity aliambia hakimu Jumatatu Feburuari 10, 2025.

Harakati za kusaka jumba la kibiashara zilimpelekea kuona kampuni moja ya mtandao kwa jina Badoo Online iliyodai ilikuwa katika biashara ya majumba na ingelimsaidia.

Purity aliambia hakimu alizungumza na mwanaume aliyejitambulisha kwa jina James.

Walijadiliana kwa muda mrefu ndipo Purity akamweleza James nia yake na pia kujituma kwake kuwekeza katika biashara ya nyumba.

James alijitolea mhanga kumsaidia lakini hakujua alikuwa akizugumza na mfungwa anayetumikia kifungo kwa ubakaji katika gereza kuu la Kamiti.

Walipoanza mazugumzo, Purity aliambia mahakama James alijitambulisha kuwa “Daktari” kwa taaluma mwenye uraia mara mbili-Mkenya/Mtanzania.

Pia alimweleza alikuwa akifanya kazi Afrika Kusini.

Hakimu alielezwa wakati Purity alikuwa wanajadiliana kuhusu ununuzi wa nyumba, James alimwambia alikuwa “katika mji wa mpakani Tarakea katika kampi ya matibabu kupambana na maradhi ya Covid.”

Purity aliambia mahakama baadaye alifahamu jina kamili ya James ni Hesbon Onyango Nyamweya.

Mahakama ilielezwa hatimaye James (Hesbon Onyango Nyamweya) aliugua na kufia katika Hospitali ijulikanayo kama Sanitas iliyoko Tanzania, kumbe ni uwongo anatumikia kifungo cha ubakaji Kamiti.

Mahakama ilielezwa Hesbon alianza kwa kutumiwa kitita cha Sh38,000 na Purity za kulipia hati zake katika afisi ya uhamiaji.

Hadi pale alipogudua anatapeliwa, Purity alikuwa amemtumia kwa mtandao wa Mpesa zaidi ya Sh7.6 milioni.

Mlalamishi alieleza korti kwamba alipiga ripoti polisi mjini Thika na kushauriwa awasiliane na maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) ambao walimtia nguvuni Hesbon.

Maafisa wa DCI kwa msaada wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom na Airtel walitambua wenye nambari za simu zilizopokea ama kutuma pesa kutoka kwa Purity.

Polisi walimtia nguvuni Pamela, mama yake Hesbon kwa kuhifadhi pesa hizo akijua zimepatikana kwa njia isiyo halali.

Wote wawili Hesbon na mama yake Pamela wamezuiliwa katika magereza ya Kamiti na Lang’ata wakisubiri kuamuliwa kwa kesi hiyo ya wizi, utapeli na kuficha pesa zilizopatikana kwa njia ya uhalifu.

Pamela amekana shtaka la kuiba Sh7,656,500 kutoka kwa Purity Karambu Laird kati ya Mei 1 na Septemba 17, 2020 mahali pasipojulikana humu nchini Kenya.

Wote wamekanusha mashtaka 12.

Kesi inaendelea.