Je, udongo wako ni salama kuzalisha chakula?
MAENEO yanayozalisha mahindi nchini yanakumbwa na changamoto kubwa ya kiwango cha juu cha asidi.
Iwapo tatizo hili halitashughulikiwa, huenda likadhoofisha juhudi kufanikisha ajenda ya kuangazia usalama wa chakula na kuondoa njaa.
Kulingana na Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), karibu asilimia 65 ya udongo wa Kenya ni wa asidi, jambo linalohatarisha shughuli za kilimo.
Kaunti ya Trans Nzoia, Uasin Gishu, Bungoma, Narok, Nakuru, Kakamega, na Nandi ndizo ngome kuu za uzalishaji wa mahindi nchini.
Hata hivyo, udongo katika maeneo haya unaendelea kuwa na kiwango cha juu cha asidi.
“Udongo unaweza kuwa na virutubisho vinavyohitajika, lakini unakosa kufanikisha kiwango hitajika cha uzalishaji chakula kwa sababu ya asidi,” asema Dkt David Kamau, Mkurugenzi wa Mazingira na Mifumo ya Rasilimali Asili KALRO.

Hilo linaashiria kuwa udongo wa Kenya haupo katika hali bora.
Changamoto hiyo imekita mizizi sehemu zinazozalisha mahindi, na pia kushuhudiwa katika maeneo kame (ASAL) ambayo yanawakilisha karibu asilimia 80 ya ardhi ya Kenya.
Kenya ina kaunti kame 23, ambapo udongo wake umeharibika kutokana na malisho ya mifugo, kwani wakazi wa maeneo haya hufuga kiwango kikubwa cha wanyama.
“Katika maeneo kame, udongo huathirika kwa sababu ya ng’ombe kung’ang’ania malisho kidogo yaliyopo,” aeleza Dkt Kamau.
Mwaka wa 2022, Kenya ilikumbwa na ukame mbaya zaidi katika historia yake, hali iliyosababisha hasara kubwa ya mazao na mifugo yenye thamani ya mabilioni ya pesa.
Sababu zingine zinazochangia udongo kudhoofika ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi, mvua ya mafuriko – inayochangia kuwepo kwa mmomonyoko wa udongo na matumizi ya pembejeo zenye kemikali.

“Wakulima wanategemea sana fatalaiza zenye kemikali, na tunawashauri washirikishe kuzichanganya na mbolea asili,” anasisitiza Dkt Kamau.
Kukabiliana na changamoto hizi, mtaalamu huyu anahimiza wakulima kuzingatia teknolojia na bunifu za kilimo endelevu ili kurejesha afya ya udongo.
Mbinu kama vile matumizi ya nyasi za mtandao, yaani mboji (mulching), kupunguza kilimo cha kina (minimum tillage), na kupanda mseto wa mimea pamoja (intercropping) ni muhimu kuboresha afya ya udongo na kuangazia kero ya usalama wa chakula hasa kipindi hiki ulimwengu unahangaishwa na athari za tabianchi.
Dkt Kamau, pia anawashauri wakulima kupima udongo wao mara kwa mara ili kuelewa hali yake.
Hata hivyo, kurejesha na kuimarisha afya ya udongo si kazi ya siku moja, mbili au tatu….
Dkt Kamau anasisitiza kuwa ni mchakato wa muda mrefu unaohitaji rasilimali za kutosha.

“Uboreshaji udongo ni zoezi linalochukua muda mrefu. Mbali na kutumia teknolojia za kilimo endelevu, tunahimiza wakulima kuongeza chokaa (lime) kwenye udongo wao,” anaelezea.
Aidha, wakulima wanashauriwa kutumia tani mbili za chokaa kwa hekta moja kila baada ya miaka miwili.
Kiwango bora cha asidi ya udongo, ni kati ya pH 6.5 na 7.5, ambacho ni wastani.
Udongo wenye pH juu ya 7.5 ni wa alkali, huku ule wenye pH chini ya 6.5 ukiwa wa asidi.
Udongo wenye pH chini ya 5.5 unachukuliwa kuwa na asidi ya juu mno.
Kwa sababu si wakulima wengi wenye uwezo kupata mbolea kwa gharama nafuu, serikali mapema 2023 ilianzisha mpango wa ruzuku ya mbolea ili kuwasaidia.

“Mpango wa fatalaiza ya bei nafuu unawapunguzia wakulima mzigo,” anasema Dkt Kamau.
Licha ya Afrika kuwa na asilimia 65 ya ardhi inayofaa kuendeleza shughuli za kilimo, na asilimia 10 ya vyanzo vya maji safi, bara hili bado linategemea sana uagizaji wa chakula kutoka nje.
Dkt Kamau anasisitiza nchi ikiwa na udongo wenye afya bora, uzalishaji mahindi unaweza kutinga magunia 45 kwa ekari kila msimu, huku wastani ukiwa magunia 30.
Hata hivyo, wakulima wengi kwa sasa wanavuna wastani wa magunia 10 pekee katika kila ekari kwa sababu ya udongo kudhoofika.
Anatahadharisha kwamba matumizi ya muda mrefu ya fatalaiza yenye Nitrojini, huchangia ongezeko la asidi shambani.
