Kaunti zisaidie kuendeleza lugha asili – Ngugi wa Thiong’o
Na WANDERI KAMAU
MWANDISHI maarufu wa vitabu, Ngugi wa Thiong’o ameziomba serikali za kaunti kuiunga Serikali Kuu mkono kutekeleza mfumo mpya wa elimu, kwani unatilia maanani umuhimu wa lugha za kiasili.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televiesheni Jumamosi usiku, Ngugi alisema kuwa kinyume na mfumo wa sasa wa 8-4-4, mfumo mpya wa 2-6-6-3 huenda ukawa mwokozi wa lugha hizo ambazo zimo katika hatari ya kusahaulika.
Hivyo, alisema kuwa magavana huwa wakawa na mchango mkubwa kuwekeza zaidi katika juhudi za kuendeleza lugha hizo.
“Magavana wanaweza kuungana kubuni mikakati ya pamoja kuendeleza lugha hizo, kwa mfano kununua vitabu na kuvisambaza katika taasisi mbalimbali za elimu. Ufanisi wa kampeni ya kuhamasisha ukumbatiaji wa lugha hizo unaweza kufana sana kwa juhudi zinazotoka mashinani,” akasema.
Msomi huyo pia aliusifia mfumo huo, akisema kuwa huenda ukawa jukwaa kuu la ufanisi wa kampeni hiyo, ambayo amekuwa akiiendeleza kwa muda mrefu.
“Mfumo huu mpya wa elimu huenda ukawa mwanzo mpya kwa kampeni za kusisitiza umuhimu wa uzingatiaji wa lugha za kiasili. Hii ndiyo changamoto kuu inayozikumba lugha nyingi asili barani Afrika na mataifa mengi yenye chumi za kadri,” akasema Prof Ngugi.
Mfumo huo ulianza kutekelezwa mwaka huu katika madarasa ya Kwanza hadi Tatu, huku ukitilia maanani uwezo wa uelewa wa mwanafunzi, kuliko ushindani kwa njia ya mitihani. Mfumo huo pia unatilia maanani ufundishaji wa lugha za kiasili kwa wanafunzi katika madarasa hayo.
Akaongeza: “Katika nchi zilizostawi, kama bara Ulaya, mojawapo ya mahitaji makuu kwa mwanafunzi anayeanza masomo yake ni kuwa na ufahamu mkubwa wa lugha yake asili, kabla ya kujifunza lugha zingine. Hili huhakikisha kwamba hakuna wakati ambapo ataisahau lugha hiyo,” akasema.
Alitaja hilo kama sababu kuu ambapo lugha kama Kiingereza, Kijerumani, Kifaransa kati ya zingine zimeendelea kusambaa duniani, huku zingine zikififia.
Mwandishi huyo aliwasili nchini mnamo wikendi kuzindua kampeni ya kutoa uhamasisho kuhusu umuhimu wa kuandika katika lugha za kiasili.
Katika ziara hiyo, Ngugi pia anatarajiwa kuzindua kitabu chake kipya: ‘Keenda Muiyuru: Rugano rwa Gikuyu na Mumbi’ (Koo Tisa: Hadithi ya Gikuyu na Mumbi) kilichoandikwa kwa lugha ya Gikuyu.
Kando na hayo, ataongoza shughuli za uzinduzi wa vitabu kadhaa vya lugha kama Kigiyrama, Kikisii, Dholuo kati ya zingine.