Habari Mseto

Wazika tofauti zao na kuunga mkono Bandari ya Dongo Kundu

February 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na HAMISI NGOWA

MBUNGE wa Likoni Bi Mishi Mboko na hasimu wake wa kisiasa Suleiman Shakombo, mwishoni mwa wiki waliamua kuzika tofauti zao na kuungana kupigia debe ujenzi wa mradi wa Bandari ya kisasa ya Dongo Kundu.

Kwa mara ya kwanza tangu kukamilika kwa uchaguzi mkuu wa 2017, wawili hao walionekana wakinong’onezana wakati ambapo wakazi walikuwa wakitoa maoni yao.

Mnong’onozano huo hata hivyo ulifungua ukurasa mpya wa siasa za eneo hilo ulipowadia muda wa viongozi hao kutoa maoni yao ambapo wote kwa pamoja waliungana katika kuupigia debe mradi huo.

Bw Shakombo ambaye alikuwa wa kwanza kuzungumza, alisema wakazi wa eneo hilo wako na hamu kubwa ya kutaka kuona mradi huo ukianza na akaiomba serikali kuharakisha utekelezaji wake.

Alisema yeye pamoja na wakazi wengine wa Mtongwe wanachokisubiri kwa sasa ni kuelezwa jinsi shughuli ya malipo ya fidia kwa waathiriwa itakavyofanyika na sehemu mbadala watakako hamishwa waathiriwa.

Alisema shughuli ya kuwafidia watakaoathirika kutokana na mradi huo inafaa kufanywa kwa haraka na kwa njia ya haki ili waathiriwa waweze kuwa na uhakika wa uwepo wa mradi huo.

Hata hivyo, alisema anaunga mkono kwa dhati ujenzi wa mradi huo pamoja na ule wa daraja kuu la Dongo Kundu akisema itabadili maisha ya wakazi wa eneo hilo.

“Tumesubiri utekelezaji wa miradi hiyo kwa kipindi kirefu lakini hatuoni ikifanyika isipokuwa vikao vya kila wakati.Naomba serikali ituambie waathiriwa watalipwa lini na wapi watapelekwa na mradi utaanza lini,’’akauliza.

Hata hivyo aliposimama ili kutoa maoni yake juu ya mradi huo,mbunge wa eneo hilo, Bi Mboko alimpongeza mbunge huyo wa zamani kwa kujitolea kwake katika kushiriki vikao vya maendeleo ya eneo hilo.

Mawazo ya Bi Mboko aidha yalionekana kuwa sawa ya Bw Shakombo aliposema kwamba yeye kama mwakilishi wa serikali kuu katika bunge la kitaifa, hangependa kuona pesa za mlipaji ushuru zikifujwa kupitia shughuli za kutathimini ufaafu wa mradi.

Bw Shakombo alikuwa amelalamikia mipango ya kurudiwa kwa shughuli hiyo ambayo alidai tayari ilikuwa imefanyika miaka mitatu iliyopita.

Hata hivyo, Bi Mboko alisema katika miradi mingi ya kiserikali inapofanyika,hali kama hiyo hujitokeza ambapo pesa za mlipa ushuru hutumika katika hali ambayo sio ya lazima.

“Naomba serikali inapofanya utathimini wake kuhusu mradi fulani basi kama ni hali ya fidia iweze kufanywa mara moja kwa kuwa shughuli kama hiyo inaporudiwa huwa ni pesa za mlipa ushuru zinazotumika,’’akasisitiza.

Bi Mboko alisisitiza haja ya viongozi kuweka tofauti zao za kisiasa kando kunapokuwa na jambo la kimaendeleo na badala yake kushirikiana akitaja kuwa hiyo ndiyo siasa komavu.

“Namshukuru mzee Shakombo kwa kuonyesha kuwa ni kiongozi aliyekomaa kwa kukubali kuungana na viongozi walioko kwenye mamlaka katika kupigania miradi itakayosaidia watu wetu,’’akasema.