Gachagua amlipukia Ruto hatima ya Jaji Mkuu Koome ikining’inia pembamba
NI roho mkononi mwa Jaji Mkuu Martha Karua na majaji sita wa Mahakama ya Juu Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) itakapokutana kesho kutoa mwelekeo kuhusu hatima yao kufuatia maombi ya kutaka watimuliwe.
Mkutano huo utaongozwa na naibu mwenyekiti wa tume hiyo Isaac Ruto na kuhudhuriwa na makamishina tisa.
Hata hivyo, Bi Koome ambaye ni mwenyekiti wa JSC na Jaji Mohammed Ibrahim, ambaye ni mwakilishi wa majaji wa mahakama ya juu katika JSC, hawatahudhuria mkutano huo kwa sababu ni miongoni mwa walengwa katika juhudi za kuwaondoa afisini.
Haya yanakuja wakati ambapo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua amemwonya vikali Rais William Ruto asidhubutu kukanyaga Mlima Kenya iwapo Bi Koome ataondolewa madarakani.
Bw Gachagua alisema baada ya kuondolewa kwake afisini, hawezi kukubali tena Bi Koome ambaye anatoka Mlima Kenya aondolewe madarakani.
“Tunakwambia Rais; wewe panga njama ufukuze Martha Koome na wewe ukae Nairobi usikanyage hapa Meru tena. Ulifukuza Rigathi Gachagua tukanyamaza ukafikiria sisi ni waoga, ukifukuza Martha Koome usikanyage hapa Meru. Sasa umezidi, unapanga njama ya kumaliza viongozi wao wale wako na msimamo na kuweka vibaraka,” akasema Bw Gachagua.
“Ama nyinyi Wameru mmekuwa waoga?” akauliza huku umati aliokuwa akihutubia ukisema ‘hapana’
Ingawa Bw Rutto alifeli kujibu simu au jumbe fupi tulizomtumia kutoa maelezo zaidi kuhusu mkutano huo, duru za kuaminika zinasema makamishna watajadili hatua watakayochukua baada ya mahakama kuu kutoa maagizo yanayozuia JSC kuendelea kushughulikia malalamishi dhidi ya Koome na wenzake.
Mnamo Ijumaa wiki jana Jaji Koome na majaji wenzake wa Mahakama ya Juu walielekea katika Mahakama ya Kuu kupinga adhabu kutolewa dhidi yao.
Walionya kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mzozo wa Kikatiba na ombwe la uongozi katika Mahakama ya Juu endapo watasimamishwa kazi kutoa nafasi kwa uchunguzi kuendeshwa dhidi yao.
Alielezea hofu kwamba endapo mahakama kuu haitatoa agizo la kusitisha hatua kama hiyo, kuna uwezekano kwamba JSC itawasilisha pendekezo kwa Rais William Ruto kwamba abuni jopo la kuchunguzi malalamishi dhidi ya majaji wote wa Mahakama ya Juu, hatua itakayositisha shughuli zote za mahakama hiyo yenye mamlaka makubwa zaidi nchini.
Akirejelea mgogoro huo wa kikatiba Jaji Koome akasema hivi: “Ni Mahakama ya Juu ndiyo yenye mamlaka ya kuhalalisha kutangazwa kwa hali hatari, uhalali wa matokeo ya uchaguzi wa urais, husikiza rufaa kuhusu kuondolewa afisini kwa majaji na hutoa ushauri kuhusu masuala mazito ya kikatiba.”
“Hakuna mtu au asasi nyingine yenye mamlaka ya kutekeleza majukumu ya kikatiba yaliyotengewa Mahakama ya Juu. Kwa hivyo, hatua ya JSC kuendelea kushughulikia maomba hayo maombi hayo itasababisha kusitishwa kwa muda kwa majukumu haya na kuwapokonya Wakenya haki zao za kimsingi,” akaeleza kwenye stakabadhi alizowasilisha kortini.
Kulingana na Bi Koome kusimamishwa kazi, kwa muda, kwa majaji wote wa Mahakama ya Juu ni kinyume cha katiba kwani “Katiba haijataja kitakachofanyika wakati ambapo Mahakama ya Juu haifanyi kazi.”
Jaji Koome anaamini kuwa maombi yaliyowasilishwa katika JSC kutaka waondolewe afisini yanalenga kusababisha ombwe katika mahakama ya juu na mzozo nchini.
Isitoshe, Jaji huyo Mkuu anasema kuwa JSC haina mamlaka ya kuhakiki utendakazi wa Mahakama ya Juu.
Maombi ya kutaka Bi Koome na wenzake sita yaliwasilishwa kwa JSC na kampuni ya Dari Limited inayomilikiwa na Waziri wa zamani Raphael Tuju na mawakili Nelson Havi na Christopher Rosana.
Wanataja mienendo mibaya, utovu wa maadili, ufisadi na utendakazi mbaya kama sababu za kutaka Jaji Koome na wenzake sababu walipigwa kalamu.
Huku malalamishi ya Bw Tuju yakihusu kuendeshwa kwa kesi kuhusu mzozo wa kibiashara kati ya Dari Limited na Benki ya East Africa Development Bank, malalamishi ya mawakili Havi na Rosana yanahusu uamuzi wa Mahakama wa Juu kumzima wakili Ahmednassir Abdullahi kuwakilisha wateja katima mahakama hiyo.
Koome na wenzake walichukua hatua hiyo kufuatia jumbe ambazo zimekuwa zikiwekwa kwenye mitandao ya kijamii na wakili Abdullahi kuichafulia jina mahakama hiyo na majaji wake.
Mahakama Kuu ilitoa maagizo ya kutaka JSC ikome kushughulikia malalamishi hayo kufuatia kesi iliyowasilishwa na Jaji Mkuu Koome, Jaji Njoki Ndung’u na Mkenya kwa jina Bw Pariken Ole Esho, kutoka Narok.
Maagizo hayo yalijiri wakati ambapo JSC ilikuwa ikitarajiwa majibu kutoka kwa majaji hao kabla ya kuyatathmini sambamba na malalamishi.
Mnamo Janujari 27, 2025, majaji hao wa Mahakama ya Juu walitakiwa kujibu malalamishi dhidi yao baada ya Kamati ndogo ya kushughulikia Malalamishi katika JSC inayoongozwa na Bw Omwanza Ombati kubainia kuwa malalamishi yaliyoibuliwa yalikuwa na mashiko.
Baada ya kuweka malalamishi na majibu mezani, kikao cha makamishna wote kingeamua kusikizwa kwa pande zote, ambapo majaji hao wangekabiliana ana kwa ana na wanaowashutumu pamoja na mashahidi.
Baadaye, JSC ingeamua ikiwa itupilie mbali malalamishi hayo au iyawasilishe kwa Rais ikipendekeza kuundwa kusimamishwa kazi kwa Koome na majaji wenzake na kuundwa kwa jopo la kuchunguza mienendo yao.
Siku ya mwisho kwa Jaji Mkuu na wenzake kuwasilisha majibu yao ilikuwa leo, Jumatatu Februari 24, 2025.