Shangazi Akujibu

NIPE USHAURI: Natafuta demu mpoa nimuoe

February 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Nina umri wa miaka 39. Ninatafuta mwanamke anayenifaa maishani kama mke. Nimewahi kuona wanawake wanaotafuta wapenzi katika ukumbi wako huu. Tafadhali nisaidie kuwasiliana nao nipate mke.

Kuna watu wanaotumia ukumbi huu kutafuta wachumba. Lakini mimi sihusiki moja kwa moja katika mambo hayo. Kama kuna mwanamke anayetafuta mume atasoma ujumbe wako huu kisha atafute namna ya kuwasiliana nawe.

Ameanza huba pembeni!

Nina mpenzi ninayempenda kwa dhati. Jambo linalonisumbua moyoni ni kwamba ana mwanawake mwingine. Nimemsikia mara kadhaa akizungumza naye kwa simu na nikimuuliza anakana. Nipe ushauri.

Nashangaa kwamba bado unaungama mapenzi yako kwa mwanamume huyo ukijua kwa hakika kuwa si mwaminifu kwako. Kuna haja gani kumpenda mtu ambaye hana haja nawe? Wanaume ni wengi. Achana naye utafute mpenzi mwaminifu.

Mpenzi wa rafiki yangu hakomi kuninyemelea

Nina miaka 24 na ninasoma chuo kikuu. Rafiki ya mpenzi wangu amekuwa akitaka tuwe na mpango wa kando. Nimemwambia siwezi lakini haachi kuniandama. Nifanye nini?

Huyo si urafiki adui mkubwa. Anajua mpenzi wako akigundua kuwa anakunyemelea watakosana na hajali. Kama umekataa ombi lake na hataki kuelewa, mwambie mpenzi wako ili amkomeshe.

Wa zamani bado anamtumia jumbe na hamkanyi

Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani kwa miaka mwili. Sasa aliyekuwa mpenzi wake ameanza kumtumia jumbe akisema bado anampenda. Nikimuuliza anasema namsumbua. Nina wasiwasi, nishauri.

Palipo na moshi pana moto na pia akufukuzaye hakwambii toka. Mawasiliano kati ya wawili hao na madai ya mpenzi wako kwamba unamsumbua kwa kumuuliza kinachoendela ni ishara kuwa wamefufua uhusiano wao. Usiendelee kupoteza wakati wako.