Habari Mseto

Spika wa kaunti ajiuzulu na kuapa kuanika gavana

Na SAMMY LUTTA February 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SPIKA wa Kaunti ya Turkana, Christopher Nakuleu, amejiuzulu kutoka afisini na kuapa kuendelea kumwangazia Gavana Jeremiah Lomorukai na bunge la kaunti.

Bw Nakuleu, aliyewahi kuhudumu kwa hatamu mbili kama mbunge wa Turkana Kaskazini, sasa anadai maswali yake kuhusu bidhaa za chakula cha msaada zilizonunuliwa na serikali ya Kaunti ya Turkana, yalimgharimu kazi ya Spika baada ya suala hilo kuingizwa siasa.

Alisema amejiuzulu kwa sababu anahisi wajibu wa Bunge la Kaunti kuhusu uangalizi umeingiliwa vibaya na gavana amekataa kuwajibikia fedha na raslimali za umma.

Wiki iliyopita, MCAs waliidhinisha hoja ya kumtimua spika wakimshutumu kwa ukosefu wa nidhamu na kazi duni.

Juhudi zake za kuzima mchakato huo baada ya kuwasilisha ombi kortini akitaka usimamishwe kwa misingi ya kukiuka taratibu za kisheria ziligonga mwamba huku idadi kubwa ya madiwani wakipitisha hoja hiyo kufuatia majadiliano mchana kutwa.

Spika Samwel Aliwo aliyeongoza kikao hicho aliagiza kubuniwa kwa kamati ya wanachama saba kuchunguza madai yaliyowasilishwa dhidi ya Bw Nakuleu katika muda wa siku saba.

Mwandani wa Bw Nakuleu, Diwani wa Lapur Michael Ewoi, aliyekuwa mwanachama wa kamati hiyo alisema mchakato wa ufurushaji ulichochewa kisiasa na matokeo yake tayari yamekadiriwa.

Spika sasa anadai masaibu yake yalianza aliposaili sababu ya maharagwe kutoweka kwenye bidhaa za vyakula vya msaada vilivyonunuliwa na serikali ya kaunti.