Jamvi La Siasa

Vinara wenza Kenya Kwanza waingiwa tumbojoto Raila akijongea serikalini

Na BENSON MATHEKA March 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

IWAPO kinara wa chama cha ODM, Bw Raila Odinga ataungana rasmi na Serikali, litakuwa pigo kubwa kwa washirika wa karibu wa Rais William Ruto hasa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na Naibu wa Rais, Prof Kithure Kindiki miongoni mwa wengine.

Muungano wa Kenya Kwanza una vyama 18 kulingana na rekodi za Msajili wa Vyama vya Kisiasa, vikiongozwa na United Democratic Alliance (UDA) chini ya Rais Ruto, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi, Ford Kenya cha Bw Wetang’ula, Pamoja African Alliance (PAA) cha Spika wa Seneti Amason Kingi na Maendeleo Chap Chap cha Waziri wa Leba Alfred Mutua miongoni mwa vingine.

Wote hao wanashikilia nyadhifa tofauti serikalini ambazo ujio wa Bw Raila na chama chake cha ODM unaweza kuwatikisa.

Wadadisi wa siasa wanasema kwamba iwapo Raila atajiunga na serikali kama Waziri Mkuu atasababisha mabadiliko makubwa ambayo yanaweza kuathiri uhusiano wa rais na washirika wake katika muungano wa Kenya Kwanza.

“Kujiunga kwa Raila katika serikali kutakuwa pigo kubwa kwa washirika wa Rais katika muungano wa Kenya Kwanza hasa Bw Mudavadi na Wetang’ula. Mudavadi yuko kwenye hatari zaidi kwa kuwa ameshavunja chama chake na kwa sasa anahudumu kwa huruma ya Rais. Wadhifa anaoshikilia pia ni wa kuteuliwa na anaweza kuvuliwa,” akasema mchanganuzi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Mnamo Januari 17 mwaka huu, chama cha ANC, ambacho Mudavadi alitumia kuunda muafaka wakati wa kubuniwa kwa muungano wa Kenya Kwanza, kilitangaza kumezwa na UDA cha Rais Ruto.

Spika Wetang’ula.

Anasema kwamba ikizingatiwa Bw Raila ni maarufu kuliko Bw Mudavadi katika eneo la Magharibi mwa Kenya, ni rahisi mbunge huyo wa zamani wa Sabatia kusukumwa kando au kupunguziwa mamlaka ili kupisha kiongozi huyo wa ODM au mshirika wake.

Baadhi ya wadadisi wanahisi kwamba akiwa mshirika mwanzilishi wa muungano wa Kenya Kwanza, Bw Mudavadi anaweza kuhisi kudunishwa iwapo hili litafanyika kwa kuwa ushawishi wake utapungua katika serikali.

“Kuna uwezakano Mudavadi, ambaye kwa sasa anahudumu kama Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni na Wakenya wanaoishi Ng’ambo, ataachiwa mojawapo ya ofisi hizo hasa hii ya Masuala ya Kigeni iwapo Raila atakubali kujiunga na serikali kwa kuwa lazima wadhifa atakaopewa kiongozi huyo wa chama cha Chungwa uafiki hadhi yake,” aeleza Gichuki.

Anasema ujio wa Raila serikalini unaweza pia kumuathiri Prof Kindiki hasa katika ubabe wa madaraka ikizingatiwa alivyoingia katika kiti hicho.“Prof Kindiki hakuchaguliwa pamoja na Rais ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Rigathi Gachagua aliyetimuliwa na hii inamkosesha nguvu katika Kenya Kwanza japo kikatiba, ndiye msaidizi mkuu wa rais,” asema.

Naibu Rais Kithure Kindiki. Picha|Maktaba

Kumekuwa na shinikizo kutoka kwa baadhi ya wanachama wa ODM, Wetang’ula atimuliwe kama Spika wa Bunge la Kitaifa wakimshutumu kwa kukaidi uamuzi wa mahakama uliofasiri kuwa Azimio la Umoja ndio muungano wa Wengi.

Wadadisi wanasema chama cha UDA hakifurahishwi na hatua ya Wetang’ula ya kukataa kuvunja chama cha Ford Kenya alivyofanya Mudavadi alipovunja chake cha ANC na ikizingatiwa wandani wa Bw Raila wamekuwa wakisukuma atimuliwe ana sababu ya kuingiwa na tumbojoto.Washirika wa viongozi hao watatu ambao wanashikilia nyadhifa za juu serikalini pia wanaweza kuathiriwa iwapo Raila na Ruto wataunda serikali ya Nusu Mkate.

Spika wa Seneti Amason Kingi. PICHA | MAKTABA

“Kuundwa kwa muungano rasmi wa kisiasa kati ya Rais Ruto na Raila kutawasukuma pembeni. Raila na Ruto watakuwa vinara wakuu katika serikali,” asema mchanganuzi wa siasa Betty Kiano.Anasema baada ya kurasmisha muungano wao, Bw Raila atapendekeza watu ambao watamsaidia kulinda maslahi yake serikalini na hii itapunguza ushawishi wa Bw Wetang’ula, Musalia na Kindiki.

“Kuna kila sababu ya vinara wenza wa Ruto katika Kenya Kwanza kuingiwa na tumbojoto kuhusu muungano ambao Raila anasuka na Ruto. “Kwa kila hali, utawaathiri na fauka ya yote ushawishi wao katika serikali utapungua,” akasema Dkt Kiano.