Habari za Kitaifa

Walimu walia shule zimesota

Na VITALIS KIMUTAI March 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SHULE zinapofunguliwa baada ya likizo fupi ya nusu muhula, maafisa wa vyama vya walimu na wakuu wa shule wameiomba serikali kutoa kwa dharura malimbikizi ya Sh64 bilioni zilizokosa kutumiwa shule.

Maafisa wa Chama cha Kitaifa cha Walimu Kenya (Knut) na wale wa Chama cha Walimu wa Shule za Sekondari na Vyuo vya Kadri (Kuppet) wanashinikiza serikali kutoa fedha hizo mara moja ili kuepusha masomo kutatizika.

Katibu Mkuu wa Knut Collins Oyuu alionya kuhusu mzozo katika shule za umma kote nchini ikiwa pesa hazitatolewa.

“Unawezaje kusimamia shule  kama mkuu wa shule bila kuwa na fedha na bajeti kutoka kwa serikali? Baadhi ya wasimamizi wa shule walilazimika kuwaachilia wanafunzi mapema kutoka shuleni kwa mapumziko ya nusu muhula na hata kuwatuma baadhi yao nyumbani kuchukua karo. Ni suala zito sana ambalo linapaswa kushughulikiwa mara moja,” alisema

“Wizara ya Elimu na Hazina ya Kitaifa zinapaswa kutoa pesa kwa wakati, ili kuruhusu usimamizi mzuri wa shule kote nchini.”

Bw Oyuu alikuwa akizungumza wakati wa mazishi ya marehemu Nancy Nampiyan Lentayaa, mamake Katibu wa Knut, tawi la Samburu Richard Lentayaa,  yaliyofanyika Losuk, eneo bunge la Samburu Magharibi.

Mwenyekiti wa Kuppet Omboko Milemba pia alionya kwamba mzozo shuleni kuhusu pesa ambazo hazijatolewa unazidi kuwa mbaya na inafaa ushughulikiwe kwa dharura.

“Ili elimu bora itolewe kwa wanafunzi wetu, tunapaswa kuhakikisha kuwa fedha zinapatikana kwa wakati unaofaa,” Bw Milemba alisema.

Wito wao ulijiri  siku chache baada ya Waziri wa Hazina John Mbadi kusema kuwa serikali haitalipa  pesa zilizolimbikiza.

Kati ya 28 bilioni za shule za sekondari, Serikali imetoa Sh14 bilioni, huku salio la Sh14 bilioni likitarajiwa kutolewa mara tu zitakapopatikana.

Lakini hatua hiyo imekasirisha vyama vya walimu na wakuu wa shule za umma, ambao wanashangaa kwa nini serikali haiwezi kuchukulia pesa za shule kama deni  kwa vile taasisi za masomo zinatarajia pesa kulipia bidhaa na huduma.

“Serikali haijatoa fedha hizo. Inadai imetoa pesa lakini haijatoa. Hazina ya Kitaifa imedai kuwa ililipa Wizara ya Elimu,  lakini haijalipa shule nah ii  imezua mzozo katika taasisi za masomo,” mkuu wa shule katika kaunti ya Samburu alisema.