SHANGAZI: Nilishindwa kuvumilia msoto nikaondoka, sasa anaposti tu magari, nimrudie?
Niliachana na mpenzi wangu wa miaka mingi kwa sababu ya umaskini. Hata hivyo, kwa sasa naona akijiposti mitandaoni akibadilisha magari tu. Je, kuna haja kurudiana naye?
Yote yanayong’aa sio dhahabu. Mambo yanayopakuliwa mitandaoni yasikudanganye, huenda anakomboa magari hayo kuvutia warembo.
Rafiki wa miaka 10 na mzee wamenisaliti
Rafiki yangu wa miaka 10 alinisaliti kwa kushiriki mapenzi na mume wangu. Alijitetea akisema mume wangu alimlazimisha. Napanga kuvunja ndoa. Naomba ushauri wako.
Uamuzi wa kuachana na mume wako ni wako. Hata hivyo, zungumza na mumeo kwanza ujue ukweli kamili. Aidha, iwe funzo kwamba usiruhusu rafiki yako awe na uhusiano wa karibu sana na mume wako.
Ghafla anabweka eti lazima nichangie mahitaji ya nyumbani
Shangazi, ni sawa mke kuchangia fedha za matumizi nyumbani? Nahisi mume wangu ananilazimisha nimsaidie kugharimia mahitaji ya familia. Nifanyeje?
Kuchangia kifedha ni suala la maelewano kati ya wanandoa. Mkae chini mzungumze na muunde bajeti uone ni wapi kila mmoja atachangia. Kusaidiana kubeba mzigo wa kifedha ni muhimu, lakini haipaswi kuwa kwa lazima itakayofanya uhisi huna amani.
Napenda muda wangu faraghani, ananishuku
Kuna jambo limenisumbua kwa muda. Kila nikitulia au kukaa peke yangu mpenzi hukasirika. Sielewi shida yake ni nini. Hataki kusikia nikimwambia niko sawa.
Jaribu kumhakikishia kwa upole kwamba hakuna tatizo lolote. Zungumza naye kwa uwazi, mueleze umuhimu wa kutenga muda wa kukaa peke yako. Kwa upande wako, msikilize ili uelewe hisia zake. Uwazi na maelewano zitasaidia kutatua jambo hili.