• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Shujaa wa vita dhidi ya ukeketaji katika jamii ya Wamaasai

Shujaa wa vita dhidi ya ukeketaji katika jamii ya Wamaasai

Na CHARLES WASONGA

HUKU ulimwengu ukiadhamisha “Siku ya Kimataifa ya Vita dhidi ya Ukeketaji (International Day of Zero Tolerance to FMG) Jumatano Februari 6, 2018,  mzee mmoja kutoka Kaunti ya Kajiado anasifika kutokana na juhudi zake za kupambana na utamaduni huu.

Daniel Sanengo Ole Pakuo ambaye ni mwanzilishi wa kikundi cha Maasai Christian Lord Ministry kinachotumia mafunzo ya Kikristo na nyimbo za injili kutoa uhamasisho kuhusu madhara ya mila hii iliyopitwa na wakati.

Alipoanzisha kampeni ya kupiga vita ukeketaji wa wasichana na ndoa za mapema katika jamii yake ya Kimaasai miaka minane iliyopita, wengi walimdhihaki na kumpuuza Mzee Ole Pakuo.

Hii ni kwa sababu wazee wa rika lake katika jamii hii bado wanaunga mkono utamaduni huu wa ukeketaji ambao hutumiwa kama ufunguo wa kuwaoza mapema wasichana ili wapate mali.

Sawa na jamii zingine za wafugaji ambazo bado zinashilikia utamaduni huu uliopitwa na wakati, wasichana huchukuliwa kama kitega uchumi ambao huozwa baada ya kukeketwa na hivyo kunyimwa nafasi ya kuendelea na masomo.

Lakini licha ya kukumbana na vizingiti si haba kutoka wenzake wahifadhina, Ole Pakuo, hakufa moyo.

Alifahamu fika kuwa juhudi zake, pamoja na watu wengine wanaopinga utamaduni huo, zingezaa matunda.

Akishirikiana sako kwa bako na wanachama wa kikundi chake ambao pia ni watu waliomkubali Kristo kuwa mwokozi wa maisha yao, mwanahakarakati huyu amekuwa akitumia nyimbo za injili kuendeleza uhamasisho dhidi ya mila hii ambayo pia ni hatari kwa afya ya wasichana.

“Desturi hizo zimepitwa na wakati. Hii ndio sababu, tofauti na wazee wenzangu, nimejitoa mhanga kuizindua wanajamii kimawazo kwa kuhamisha kuhusu madhara ya mila hii,” asema mzee huyu ambaye ni mcheshi.

Anazidi kuarifu kwamba, tangu alipoanzisha jitihada hizi amezuru maeneo kadhaa katika janibu za Wamaasai akiendesha kampeni za kuwaelimisha wanajamii kuhusu athari za mila hiyo. Amefaulu kuwakomboa wasichana wengi na kuwawasilisha kwa Shirika la World Vision ili warejeshwe shuleni.

”Elimu ndio msingi wa maisha. Ndoa za mapema na ukeketaji wa wasichana wetu ni desturi ambayo imepitwa na wakati kando na kuwa hatari kwa maisha ya wasichana wetu. Hii ndio maana mimi na wenzangu katika Maasai Christian Lord Ministry hufanya juu chini kuwakomboa wasichana na kuwawasilisha kwa World Vision wafadhiliwe kimasomo,” asema Ole Pakuo.

Kulingana na Bw Moses Chepkonga ambaye ni meneja wa masuala Elimu na Utunzaji katika World Vision licha ya kampeni zinazoendesha na makundi mbalimbali ukeketaji, wasichana bado unaendelea katika baadhi ya jamii za humu nchini.

“Kulingana na Takwimu kuhusu Masuala ya Afya (Kenya Health Demographic Survey) ya mwaka wa 2017, asilimia 24 ya wanawake kati ya umri wa kati ya miaka 15 na 45 wamekeketwa chini. Na jumla ya wasichana 200 milioni kote duniani wamepitia kisu cha ngariba,” anasema Bw Chepkonga.

Mzee Ole Pakuo anasema kuwa tangu alipoanzisha kampeni hiyo yeye na wanachama wa kikundi chake wamefaulu kuwasaidia zaidi ya wasichana 300 kuepuka kisu cha ngariba katika kaunti za Kajiado, Laikipia na Narok.

“Haikuwa kazi rahisi. Tulikumbana na upinzani mkali mno kutoka kwa wazazi wa wasichana hao. Nusra wengine watudhuru lakini Mungu amekuwa kinga na mlinzi wetu katika kampeni hizi,” anasema.

“Aidha, tumeweza kuguza nyoyo za wengi kutokana na hali kwamba tunatumia nyimbo, sanaa na uigizaji zenye maudhui ya kidini kupiga vita uovu huu,” Ole Pakuo anaoengeza, akisisitiza kuwa mafunzo yao huangazia athari za ukeketaji kama matatizo yanayowakumba wasichana wanapojifungua.

Hitilafu hizo, kama vile, kuvuja damu kupita kiasi wakati wa kukeketwa husababisha maafa, anafafanua.

Baadhi ya vibao ambavyo amewahi kutunga ni kama vile “Nkuya Aburam” (yaani, Baba Yetu Abrahamu), “Osaya le Ngai (Maombi kwa Mungu), “Olesho lai enukoenkai” (tumkubali Mungu katika taifa letu), kati ya vingine.

Mzee Ole Pakuo alizaliwa mnamo mwaka wa 1956 katika eneo la bunge la Kajiado ya Kati.

Kwa ilivyo kawaida kwa vijana wengi wa jamii hiyo nyakati hizo, hakujiunga na shule yoyote, badala yake, aliingilia shughuli za kuchunga ng’ombe na kondoo.

Na alipokuwa na umri wa miaka 18 talanta yake ya uimbaji ulianza kuota. Alighani nyimbo za kitamaduni ambazo zilimpa sifa si haba miongoni mwa vijana wenzake.

”Nilikuwa nikialikwa kutumbuiza katika dhifa na sherehe mbalimbali kama vile tohara, ndoa kati ya zingine.

Mnamo 2001, Ole Pakuo alikata kauli kumkubali Yesu kama mwokozi wa maisha yake na akaanza kampeini za kupiga vita mila na desturi zinazodhalilisha utu.

Ana mpango wa kuanzisha kituo cha kuwafaa kielimu, kiroho, kimaadili na kiuchumi wasichana waliookolewa kutoka kwa kisu cha ngariba na ndoa za mapema.

You can share this post!

Huduma Centre ya Thika sasa kuhudumia wananchi kuanzia...

Salah aibuka mchezaji bora wa EPL tena

adminleo