Kindiki aahidi bei ya juu ya kahawa huku akitwaa ‘mageuzi’ yaliyokuwa ya Gachagua
NAIBU Rais Kithure Kindiki amewahakikishia wakulima wa kahawa kwamba mapato yao yataimarika mwaka huu kutokana na mipango inayotekelezwa na serikali katika sekta hiyo.
Prof Kindiki ambaye amechukua wajibu wa kuongoza mageuzi katika sekta hiyo, uliotekelezwa na mtangulizi wake Rigathi Gachagua, alisema kilo moja ya kahawa inatarajiwa kuuzwa kwa Sh110 mwaka huu.
Hii ni bei bora kuliko bei iliyokuwepo kabla ya serikali ya Kenya Kwanza kuingia mamlakani mnamo 2022.
Kufufuliwa kwa sekta ya kahawa kulikuwa mojawapo ya ahadi ambazo Rais Ruto na Bw Gachagua walitoa kabla na baada ya kuingia mamlakani.
Hii ndio maana katika agizo nambari 1 alilotoa Oktoba 2, 2022, Rais Ruto alimpa Bw Gachagua kibarua cha kuongoza mageuzi katika sekta za kahawa, majani chai na maziwa.
Mnamo 2023, Bw Gachagua aliandaa mkutano mkuu wa madai katika sekta ya kahawa katika Kaunti ya Meru kujadili changamoto zinazosibu maendeleo katika sekta hiyo.
Ajenda kuu ya kongamano hilo ilikuwa kuibua na kujadili mapendekezo yanayolenga kuimarisha ukuzaji wa kahawa.
Jana, Prof Kindiki alikutana na muungano wa wabunge kutoka maeneo kunakokuzwa kahawa katika makazi yake rasmi mtaa wa Karen, Nairobi kujadili mageuzi katika sekta husika za kilimo.
Prof Kindiki alisema kupanda kwa bei ya kahawa kumechangiwa na mageuzi kadhaa na mikakati inayotekelezwa na serikali katika sekta hiyo kwa manufaa ya wakulima.
“Sharti tuhakikishe mapato ya wakulima wa kahawa yanaimarika na zao hili linatuletea fedha zaidi za kigeni. Manifesto ya Kenya Kwanza inatuhitaji kuhakikisha kuwa mapato ya wakulima wetu yanaimarika. Tunatekeleza manifesto hiyo na kuhakikisha kuwa wakulima wa kahawa wanapokea angalau Sh100 kwa kilo ya kahawa,” akasema.
Naibu Rais aliwataka wabunge kuharakisha kupitishwa kwa Mswada wa Kahawa wa 2023 na Mswada wa Vyama vya Ushirika wa 2024. Miswada hiyo ingali katika Seneti baada ya kupitishwa katika Bunge la Kitaifa.
Alitaja miswada hiyo kama nguzo ya ufanisi katika juhudi za kuhakikisha kuwa mapato ya wakulima wa kahawa yanaimarika zaidi.
“Miswada hiyo sharti ikamilishwe haraka iwezekanavyo kwa sababu ni muhimu katika kufanikisha mageuzi katika sekta hiyo. Tunahimiza Seneti kukamilisha sheria hizo ili kufanikisha mageuzi katika sekta ya kahawa,” akasema.