Salah aibuka mchezaji bora wa EPL tena
NA CECIL ODONGO
FOWADI matata wa Liverpool Mohamed Salah kwa mara nyingine tena ameibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL) wa mwezi Januari, 2019.
Raia huyo wa Misri hata hivyo alitolewa kijasho chembamba na wapinzani David de Gea, Paul Pogba, Marcus Rashford, Troy Deeney na Leroy Sane kabla ya kutwaa tuzo hiyo kwa mwezi wa pili mfululizo.
Salah alifunga mara tatu katika mapambano manne ya haiba mwezi Januari na kuisaidia The Reds kusalia kileleni mwa jedwali la EPL na pia kuendelea kuongoza orodha ya wafungaji bora msimu wa EPL mwaka wa 2018/19 unapoendelea kupamba moto.
Mwanadimba huyo anaongoza orodha ya wafungaji baada ya kucheka na nyavu za wapinzani mara 16 baada ya raundi 24 ya mechi za ligi hiyo.
Mshambulizi huyo hata hivyo atalenga kuitafutia timu yake magoli kwenye mechi dhidi ya WestHam jijini Londom usiku huu wa Februari 4, 2019 .
Uongozi wao kileleni mwa EPL ulikatwa hadi alama mbili kutokana na ushindi wa 3-1 wapinzani wao wakuu Manchester City walisajili dhidi ya Arsenal Jumapili Februari 3.
Westham wanaoshikilia nafasi ya 12 kwa alama 31 watalenga kuiadhibu Liverpool ili kujitoa katika mduara wa timu zinazokabiliwa na hatari ya kushushwa ngazi.
Ushindi utawapaisha hadi nafasi ya nane, alama nne tu nyuma ya nambari saba Wolvehampton Wanderers ambao wametesa sana msimu huu.