Jamvi La Siasa

Waziri wa Ulinzi ambaye aliwahi kuwa dereva wa basi jijini

Na KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK March 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KANDO na kufanya kazi ya ukarani kwa muda mfupi katika miaka miwili kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Fort Hare Afrika Kusini 1948, baada ya kutoka Shule ya Upili ya Alliance 1945, John Njoroge Mungai alikuwa dereva wa basi, akiwasafirisha abiria kati ya Limuru na Nairobi.

Mungai ambaye baadaye alikuwa Waziri wa Ulinzi alikumbuka: “Nilipata leseni yangu ya kuendesha Magari ya Uchukuzi wa Umma (PSV) mwaka wa 1946, ambayo nakala yake bado ninaihifadhi. Nilikuwa nikiendesha basi la Chevrolet lenye viti 60 kati ya Limuru na Nairobi kupitia Kikuyu. Kabla ya hapo, nilifanya kazi kwa muda mfupi katika Shirika la British Overseas Airways.”

Mungai alizaliwa katika kijiji cha Gichungo kando ya mpaka wa Nairobi na Kiambu mnamo Januari 7, 1926, na wazazi Wakristo, George Njoroge Singeni ole Mbachucha na Leah Gathoni wa Kungu wa Magana.

Babake alitoka Narok na mamake alitoka Gatundu. Nyumba ya familia yake ilikuwa ikitumiwa kwa siasa na hata kabla Mungai kuzaliwa, siasa za wakadamizaji na waliokadamizwa zilikuwa katika eneo lao.

Nyumba hiyo ilihifadhi wale wote waliotetea haki na maadili ya Kiafrika, kama vile Waiyaki wa Hinga, na ‘mtumishi wa wakandamizaji wa kikoloni’ kama Chifu Mkuu Kinyanjui wa Gathirimu. “Kuwa kati ya pande mbili zilizopingana ilivutia. Siasa zinazohusu ardhi, elimu na dini zilikuwa utaratibu wa kila siku,” anasema.

Anakumbuka kuambiwa jinsi John William Arthur, msimamizi wa ukoloni wa Kanisa la Scotland huko Kikuyu, alijaribu kuwalazimisha wenyeji kuacha mila na tamaduni zao na kufuata za kigeni.

“Kwa kweli, kulikuwa na upinzani kutoka kwa wale ambao hawakuona mgongano kati ya Ukristo, elimu, maisha ya kisasa na mila na tamaduni zao,” Mungai anasema. Ingawa huenda desturi fulani hazikufaa, mtazamo wa Arthur ulizua mzozo na mgawanyiko wa watu na wafuasi wa kanisa.

”Kundi lililogawanyika, lililoongozwa na Gatungu Gathuna, lilijitenga na dini na kuanzisha shule za kujitegemea zinazojulikana kama Gikuyu Karing’a.Mungai anakumbuka: “Mfumo huu wa elimu baadaye ulizaa wapiganiaji wa uhuru. Wale waliojitenga na Kanisa la Scotland wakawa wapiganiaji wa ardhi iliyotwaliwa na wakoloni na vita vya uhuru,” alikumbuka Mungai.

Sababu moja ambayo huenda ilichangia chaguo la Mungai la kazi baadaye maishani inaweza kuwa ukweli kwamba alizaliwa hospitalini wakati ambapo, kwa Waafrika, kujifungulia nyumbani kulikuwa kawaida na ilikuwa vigumu kwenda hospitalini kujifungua.

Alieleza : “Mama yangu alikuwa miongoni mwa wanawake wa kwanza kwenda shule na kujifunza kusoma na kuandika. Yeye na baba yangu walikuwa washiriki wa Kanisa la Mwenge, Kikuyu, ambako kumbukumbu za kuzaliwa kwangu zilihifadhiwa. Rekodi hizo bado ziko Kanisani na zinaonyesha kuwa mkunga wangu alikuwa Dkt John William Arthur.”

Wazazi wake walikuwa Wakristo waaminifu na Mungai alibatizwa mwaka uleule aliozaliwa na katika Kanisa la Torch.