Habari Mseto

'Al Shabaab' 17 waachiliwa huru

February 5th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MAHAKAMA moja ya Kwale imewaachilia huru vijana 17 ambao walikuwa wameshtakiwa kwa kujihusisha na kundi la kigaidi la Al Shabaab, baada ya ushahidi kukosekana.

Vijana hao walikuwa wakikumbana na mashtaka ya kuwa wanachama wa kundi hilo na kupatikana na bidhaa ghushi.

Lakini akitoa uamuzi wa korti Jumatatu, Hakimu Mkuu Dominica Nyambu alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kutoa ushahidi wa kutosha dhidi ya washukiwa.

Washukiwa hao walikuwa wa kati ya umri wa miaka 18 na 27 na walikamatwa mnamo Januari 28, 2019 katika nyumba moja eneo la Samburu, kaunti ya Kwale.

Walipinga mashtaka na kudai kuwa walikuwa wauzaji waliokuwa wameajiriwa na kampuni ya Primmax Limited, ambayo ina matawi kadha eneo pana la Pwani.

Vitambulisho vyao vilionyesha kuwa wanatoka kaunti za Tana River, Kilifi, Nakuru, Baringo na Kisii.

Kuachiliwa kwao kumekuja siku chache tu baada ya mahakama ya Nyeri aidha kuwaachiliwa washukiwa wa shambulizi la Dusit D2 wiki chache zilizopita kwa ukosefu wa ushahidi.

Abdul Kibiringi, James Mwai na Habiba Hunshur walifikishwa kortini kwa mara ya kwanza Jumatatu iliyopita baada yao kukamatwa, lakini waliporejeshwa kortini baadaye ushahidi ukakosekana.