• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 11:28 AM
Gavana azindua barabara ya lami kuwafaa wakulima

Gavana azindua barabara ya lami kuwafaa wakulima

NA RICHARD MAOSI

GAVANA wa Nakuru Bw Lee Kinyanjui amezindua miradi ya maendeleo katika eneo la Subukia, Kaunti ya Nakuru.

Akiandamana na naibu wake Dkt Erick Korir walizindua mradi wa kutengeneza barabara inayounganisha Nakuru na Nyahururu.

Njia yenyewe ilikuwa katika hali mbaya na inakusudia kurahisisha uchukuzi wa bidhaa kutoka mashinani hadi kwenye maeneo ya kibiashara yanayozunguka Subukia.

Mradi wenyewe aliupatia jina la ‘Boresha Barabara’ kama njia mojawapo ya kutimiza ahadi alizokuwa amewapatia wakazi 2018.

“Siku za mbeleni wakulima walikuwa wakipitia wakati mgumu kufikisha bidhaa zao sokoni. Katika ajenda zangu kuu nitahakikisha raia wanaboreshewa huduma,”alisema.

Aidha aliongezea kwamba baadhi ya hatua zimeanzishwa ili kurekebisha njia nyingine zenye hitilafu katika kaunti.

Gavana akipanda mti katika hospitali ya Subukia Sub-County siku ya Alhamisi. Picha/Richard Maosi

Baadaye alifululiza hadi kwenye kituo cha Subukia Youth Hub kukagua ubunifu miongoni mwa vijana.

Vijana wengi wamekuwa wakitumia mtandao kujipatia ajira na kurahisisha maisha kupitia uvumbuzi wa kiteknolojia.

Kufikia 2019 vijana 174 kutoka kaunti jirani walikuwa wamepitia taasisi yenyewe na kuhitimu baada ya kujipatia ujuzi wa kufanya kazi kwenye mtandao.

Simon Mugo mwasisi wa Youth Hub alieleza mafanikio makubwa kutokana na juhudi za vijana kuonyesha kiu ya kujiendeleza.

“Wengi wao wamefaulu na kuwapokeza wenzao ujuzi wa kitaaluma ili kuzima harakati zao kutafuta kazi,”alisema.

Youth Hub ni kituo kinachopata mtandao kupitia wizara ya ICT.

Pia alitembelea hospitali ya Kaunti Ndogo ya Subukia kuchunguza huduma za wauguzi.

Aliahidi kuongeza idadi ya wauguzi,kando na kukabiliana na wanyakuzi waliokuwa wakivizia Ardhi ya hospitali.

Alisema ameanzisha mchakato wa kupanua wadi ya akina mama na kuongeza idadi ya wafanyikazi katika kituo cha kutoa nasaha hospitalini.

You can share this post!

‘Al Shabaab’ 17 waachiliwa huru

China yazindua apu inayotambua mtu wa madeni akiwa karibu

adminleo