Maoni

NASAHA ZA RAMADHANI: Kufuturishana wakati wa saum ni kwa ajili ya kuleta usawa, thawabu

Na ALI HASSAN March 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ASSALLAM Aleykum. Ewe ndugu yangu muumin wa dini yetu tukufu ya Kiislamu. Angalia jinsi ambavyo Mola wetu alivyotuambia kuwa funga ya saumu ni siku chache mno kwenye kitabu chetu kitukufu cha Kurani.

Hapa tunaamanisha kuwa ndugu zangu waumini wa dini ya Kiislamu tumeanza juzi tu mfungo wa Ramadhani na sasa tupo kwenye mikimbio ya kati kati ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Sisi waumini tunatakiwa kulishana kwenye mfungo wa mwezi huu. Maskini kwa matajiri inafaa kulishana. Kulishana huku ama kufuturishana tumehimizwa kufanya hivyo ili kuleta usawa na pia kuvuna thawabu. Aidha, Mola wetu Mtukufu ametueleza ni kina nani wanaotakiwa kufunga na ni kina nani wasiotakiwa kufunga na wafanye nini.

Anasema Mwenyezi Mungu mwingi wa neema na rehema:

(Mfunge) siku maalumu za kuhisabika. Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine. Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini. Na atakaye fanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ni bora kwenu, kama mnajua.

Aidha, ni vizuri hapa kukumbushana kuwa kufuturishana kunaweza kuwa ama kwa tende au maji. Uzuri wa dini yetu ni kuwa anayefuturisha na huyo mwenye kufuturishwa wote wanavuna thawabu. Raha iliyoje ndugu yangu muumin wa dini hii tukufu ya Kiislamu.

Kadhalika, kwetu sisi waja kulishana inatufanya kuwa na usawa. Usawa huu ukimfanya tajiri kuyajua makali ya njaa. Hivi kwamba hata baada ya mfungo wa saum, tajiri anaelewa makali ya njaa. Akiombwa na maskini anaelewa.