Dondoo

Mshereheshaji asiyetaka kulipa deni aaibishwa kazini

Na SAMUEL MUIGAI March 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Ndeiya, Limuru

FUNDI mmoja alimuaibisha MC maarufu mbele ya umati alipomdai deni lake hadharani.

Kulikuwa na sherehe kijijini huku na kutokana ucheshi wake, polo akapewa jukumu la kuongoza shughuli za siku kama MC.

Aliendesha Sherehe vizuri na kila mmoja aliyehudhuria akafurahia.

Wakati wa wageni wa kutoa shukran ulipofika, mmoja wao alitoa noti kama njia ya kumtunuku MC kwa kazi nzuri.

Papo hapo, fundi aliyekuwa ameketi kwenye umati alinyanyuka na kusema kwa sauti.

“Aiseh, umekuwa ukinizungusha kila ninapokudai. Sasa umepewa pesa nikiona, utaniambia nini sasa?”

Hii ilimfanya aliyekuwa MC stadi kugeuka kigugumizi. Alijaribu kumtuliza fundi lakini fundi hakuwa tayari kusikiza chochote.

Ilibidi mgeni mmoja ajitolee na kumlipia MC deni lake ili kumuondolea aibu zaidi.