Pasta ashtakiwa kuhepesha sadaka ya Sh23.5 milioni
PASTA Daniel Busheni Munalo wa Kanisa la Word of Life Centre amefikishwa mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bi Dolphina Alego akikabiliwa na mashtaka manne ya uhalifu.
Munalo alikabiliwa na mashtaka manne ya wizi na ughushi wa barua za kubadilisha majina ya watu wanaopasa kutoa pesa za kanisa hilo katika benki.
Munalo alidaiwa alitekeleza wizi huo katika kipindi cha miaka miwili kati ya Novemba 1 2019 na Agosti 9 2021.
Hakimu alifahamishwa na kiongozi wa mashtaka kwamba alitekeleza wizi huo baada ya kupokea pesa hizo kutoka kwa wafadhili wa kanisa hilo walioko nchini Canada.
Bi Alego alielezwa kuwa Munalo ni mmoja wa majenti wa kanisa hilo la Word of Life Church wanaoruhusiwa kusimamia na kuendeleza miradi ya kanisa hilo.
Bi Alego alielezwa kuwa pesa alitumiwa kutoka Canada za kugharamia ujenzi wa miradi mbali mbali ya kanisa hilo.
Baadhi ya pesa hizo zilikuwa zinunue ardhi ya kujenga kanisa.
Pasta huyo alidaiwa alikwenda katika Benki ya Eco Bank iliyoko Eco Bank Towers kaunti ya Nairobi na kuwasilisha kwa Meneja wa Benki Eco Bank ombi la kufanyia marekebesho wanaopasa kuzipokea pesa na kuzitoa.
Wakili Kavutha Muthama anayemwakilisha Pasta Munalo aliomba aachiliwe kwa dhamana huku akidai “mshtakiwa anateswa tu kama vile Mtume Paul.”
Bi Muthama alisema kanisa hilo liko na mapasta saba na watano wamekuwa wakitia sahini akaunti za benki hiyo na kutoa pesa za huduma.
Bi Muthama alisema mshtakiwa hana budi ila kufika kortini wakati wa kusikizwa kwa akaunti.
Kiongozi wa mashtaka hakupinga ombi hilo.
Mshtakiwa aliachiliwa kwa dhamana ya Sh2 milioni pesa tasilimu.
Kesi hiyo itatajwa tena Machi 27, 2025 kupewa mwelekeo mpya.